Mratibu wa mafunzo na Kaimu Mtiva wa Kitivo cha Sayansi za Jamii Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Harlod Utouh akitoa mafunzo kwa Wakulima wa Kijiji cha Changarawe.
Wanakijiji wa kijiji cha Changarawe na Wataalamu wa Chuo Kikuu Mzumbe wakifuatilia mafunzo
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa jamii na Ushirikishwaji, Dkt. Isaya Lupogo akizungumza na Wakulima wa Kijiji cha Changarawe
Washiriki wa mafunzo wakichangia maoni yao wakati wa mjadala
Bibi Shamba wa Kijiji cha Changarawe, Bi. Beatrice Byoma, akiwafundisha kwa vitendo wakulima hao jinsi ya kupanda kitaalamu mbegu za Alizeti
Wakulima wakiaandaa mbegu katika shamba la mfano kwenye mafunzo hayo
Wakulima wakisia mbegu katika shamba la mfano kwenye mafunzo hayo
Mratibu Msaidizi wa mafunzo, Bi. Felister Tibamanya, akiwaelekeza jambo wakulima katika shamba la mfano
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na Wakufunzi wa mafunzo
…………………………………
Wakulima wa Kijiji cha Changarawe kilichopo Kata ya Mzumbe, wamepatiwa mafunzo ya kilimo biashara yatakayowawezesha kulima kwa tija zao la Alizeti kwa kuliongezea thamani pamoja na kuelekezwa hatua za upatikanaji wa masoko ikiwa ni pamoja na kujiunga katika vikundi vya ushirika.
Hayo yameelezwa Dkt. Harlord Utouh, Mtiva wa Kitivo cha Sayansi za Jamii na Mratibu wa mafunzo, wakati wa mafunzo yaliyofanyika Kampasi Kuu Morogoro – Maekani.
Dr. Utouh amesema, chuo kimeamua kutoa mafunzo hayo ya kilimo endelevu cha biashara ili kuisaidia jamii inayokizunguka kuachana na kilimo cha kujikimu na kujikita kwenye kilimo biashara kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kuboresha Maisha yao.
“Kama chuo tunawajibu wa kuisaidia jamii inayotuzunguka ili ifaidike na uwepo wetu hapa. Tumefanya utafiti na kubaini fursa za kiuchumi zilizopo katika jamii hii na tumeona kilimo cha Alizeti kina thamani kubwa, lakini hakifanyiki kwa tija.
Hivyo tumechukua jitihada za makusudi kuwasaidia wakulima hawa kwa kuwafundisha mbinu bora za kilimo cha kisasa kwani zao la Alizeti ni kati ya mazao muhimu ya biashara nchini”. Alisisitiza Dkt. Utouh
Ameongeza kuwa washiriki waliopatiwa mafunzo hayo wataendelea kulelewa na Chuo Kikuu Mzumbe, kwa kuanzishiwa shamba darasa la mfano lengo likiwa ni kuwafundisha wakulima wengi zaidi kujiunga na kilimo cha Alizeti, pamoja na kujiunga katika vikundi na kutengeneza vyama vya ushirika ili kurahisisha upatikanaji wa soko la uhakika.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa kijiji cha Changarawe, Bi. Christina Nyamhaga, amekipongeza na kushukuru uongozi wa Chuo kwa kuwapatia mafunzo hayo, na kueleza kuwa yamewasaidia kujifunza mbinu mpya na bora ambazo hawakuzijua hapo awali, na kwamba mafunzo hayo yatawawezesha kuanza kilimo cha Alizeti kwa wingi tofauti na awali.
“Nimefurahi sana kupata mafunzo haya kwani ninakipenda kilimo cha Alizeti lakini sikuwa na utaalamu. Kwa mafunzo haya tunakwenda kuwafundisha na wenzetu na kuwaelimisha tujiunge kwenye vikundi ili kufanya kilimo cha ushirikiano kwani tulishajaribu kufanya mmoja mmoja lakini hatukufanikiwa:Alisema.
Shamba hilo la mfano, nimeanzishwa katika kijiji cha Changarawe kwa uratibu wa Bibi Shamba, Bi. Beatrice Byoma, na umelenga wanakijiji wote wanaoishi katika kijiji hicho wakiwemo vijana ambao kwa muda mrefu wameonekana kulalamika kukosa ajira.
Chuo kimeahidi elimu ya kilimo cha Alizeti na masoko kitakuwa endelevu, kwa kuanza na kijiji cha Changarawe na baadae elimu hiyo itaenea katika vijiji vingine vinavyozunguka chuo hicho.