Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuthamini kazi zinazofanywa na walimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuwapatia vishikwambi kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wao.
Pongezi huzo zilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Prisca Myalla alipokuwa akiongelea mchango wa walimu wanawake katika divisheni yake ofisini kwake jana.
Mwalimu Myalla alisema “kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Mhehsimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini kazi ya ualimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Nasema hivyo, kwa sababu walimu wote wamekabidhiwa vishikwambi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia. Tunaishukuru sana serikali kupitia mabadiliko ya sayansi na TEHAMA yatarahisisha zoezi la ufundishaji kwa walimu wetu na kuongeza ari ya uwajibikaji”.
Mwalimu Myalla alisema kuwa siku ya wanawake duniani ni muhimu kwa kada hiyo yenye watumishi wengi wanawake. “Hivyo, ni jeshi kubwa katika divisheni yangu kuhakikisha kwamba hali ya elimu ya awali na msingi inasimamiwa na wanawake zaidi ili iendelee kuwa bora zaidi. Ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke ndiye anayefanya dunia iwepo. Hivyo, thamani yao ni kubwa. Mwanamke ndiyo mlezi wa familia, jamii na taifa” alisema Mwalimu Myalla.
Akiongelea shughuli zilizofanywa na divisheni yake kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani, alizitaja kuwa ni kupanda miti katika viunga vya shule za msingi katika jiji hilo. “Shughuli nyingine ni kuwatembelea wanawake wenzetu waliofungwa katika gereza la Isanga kwa lengo la kuwatia moyo na kuwakumbusha kuwa thamani yao bado ni kubwa kama wanawake pamoja na kuwa gerezani. Pia tulitembelea makao ya watoto kupeleka zawadi na misaada mbalimbali” alisema.
Ikumbukwe kuwa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma inasimamia jumla ya shule 158, kati ya hizo shule za serikali ni 99. Aidha, divisheni ina watumishi 1,857 kati yao watumishi wanawake ni 1,451.