Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mheshimiwa Jaffar Haniu amekabidhi leo jumla ya pikipiki 61 kwa Maafisa Ugani katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Akikabidhi pikipiki hizo, Mhe Haniu amewagiza watalamu hao wa kilimo kwenda na kushiriki ipasavyo katika usimamizi na uzalishaji wa mazao ya kilimo ikiwa ni mbinu bora kuongeza kipato cha kaya na lishe kwa jamii.
Aidha ameagiza pikipiki hizo kutumika kwa malengo mahususi yaliyokusudiwa ikiwa ni nyenzo sahihi ya kuwafikia wakulima kuanzia ngazi ya shina, Kitongoji hadi kijiji.
“Tahadhari msiende kutumia pikipiki hizi kama bodaboda mtakuwa mnakiuka malengo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wakulima wanapata ushauri wa kitaalamu na kwa wakati” Ameongeza Mhe.Haniu.
Akishukuru kwa niaba ya maafisa ugani, Jenister Munisi mtaalamu wa kilimo kutoka kata ya Kinyala amemshukuru Mhe. Rais kwa maamuzi thabiti aliyoyafanya na kuwa wataenda kutekeleza kwa vitendo zoezi la uzalishaji wa mazao ya chakula biashara kwa ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.