………….,…….
Na Mwandishi wetu, Babati
UONGOZI wa shule ya awali na msingi Tarangire ya Mjini Babati Mkoani Manyara, umeeleza kuwa wanafunzi wa shule hiyo wanafanikiwa kufanya vyema kwenye mitihani yao kutokana na wanafunzi, wazazi na walimu kushirikiana kama timu.
Mkurugenzi wa shule hiyo Ronald Paul ameyasema hayo wakati Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange akitoa zawadi na vyeti ikiwemo fedha taslimu kwa walimu 60 wa shule 16 za msingi na sekondari zilizoongoza kwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha pili na cha nne.
Mkurugenzi huyo Paul amesema siri kubwa ya mafanikio ni ushirikiano wa pamoja na kuwajali watumishi wa shule hiyo ambao ndiyo wanaishi na wanafunzi kila siku shuleni.
“Tunawapenda wanafunzi wetu na tunawapa huduma bora na kuwaandalia mazingira mazuri ya kujiamini zaidi katika kufanya mitihani, ndiyo siri kubwa ya ufaulu kwao,” amesema Paul.
Katika hafla hiyo, shule ya awali na msingi ya Tarangire imetunukiwa zawadi na mkuu wa wilaya ya Babati baada ya kuibuka tena kidedea katika matokeo ya darasa la saba Mwaka 2022 na kuzipita shule kongwe katika halmashauri ya mji wa Babati.
Zawadi hizo ni pamoja na cheti na fedha taslimu shilingi 120,000, ambapo mwalimu wa shule hiyo Mandela Msilu alibuka kidedea kwa kuongoza katika somo la kiswahili na kupata zawadi ya cheti na Shilingi 50,000.
Masomo mengine ambayo shule ya Tarangire imefanya vizuri mno katika mtihani huo ni kingereza, hesabu, sayansi na maarifa ya jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa White Rose, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro John Don Twange amezisifu shule za Wilaya ya Babati kwa kufanya vizuri katika mitihani hiyo hususan shule ya Tarangire na kusema anatembea kifua mbele kwa kuwa wilaya anayoisimamia inafanya vizuri katika sekta ya elimu.
Twange amesema lengo la hafla hiyo ni kuongeza hamasa ya walimu hao kufanya vyema zaidi na kuiendeleza Babati katika kuifanya kuwa kinara katika suala zima la sekta ya elimu.
“Asanteni sana walimu kwa kufanikisha ufaulu mzuri ndiyo sababu tukaona ni vyema kuwashika mkono na kuwapongeza ili kuwapa moyo ila msibweteke endeleeni kufundisha vyema zaidi,” amesema Twange.
MWISHO