Na Mwandishi wetu, Babati
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi, Wilaya ya Babati Mjini Mkoani Manyara, Emmanuel John Khambay, ataipatia meza 20 na viti 20 shule ya sekondari Komoto kutokana na ufaulu mzuri wa matokeo ya kidato cha pili na cha nne.
Khambay ametoa ahadi hiyo kwenye hafla ya utoaji wa zawadi katika shule ya Sekondari ya Komoto kwa kufanya vizuri, miaka minne mfululizo kwa kuondoa daraja la sifuri.
Mwenyekiti huyo wa jumuiya ya wazazi, Khambay ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika shuleni hapo na amegawa zawadi mbalimbali kwa walimu na wanafunzi.
Ameupongeza uongozi mzima wa shule hiyo, chini ya usimamizi wa mkuu wa shule hiyo Denis Bakuza na uongozi wa bodi ya shule hiyo inayoongozwa na komredi Mahenge.
Khambay amewaahidi viongozi wa shule hiyo na bodi nzima ya shule kuendelea kuwa na ushirikiano nao ili kuendeleza kupata matokeo mazuri zaidi kwa wanafunzi.
“Nawaahidi viongozi wa shule, kwenye suala la maendeleo mimi nipo tayari muda wowote kujitoa kwa chochote nilichojaaliwa kwa manufaa ya jamii,” amesema Khambay.
Amesema yeye kama Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi pia jukumu lake kubwa ni kuwa mlezi wa watoto na anajua kuwa uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi na yeye ndiyo mzazi.
Hata hivyo, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za kuwajengea madarasa saba mapya na jengo la utawala kwenye shule hiyo ya sekondari Komoto.
Mkuu wa shule ya sekondari Komoto, mwalimu Denis Bakuza amemshukuru Khambay kwa kujitolea meza hizo 20 na viti 20 ambavyo vitawasaidia wanafunzi wa shule hiyo kuvitumia.
“Umedhihirisha kauli mbiu ya jumuiya ya wazazi kuwa uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi, tunakushukuru mno kwa kutuzawadia samani hizo,” amesema mwalimu Bakuza.