Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
ABIRIA waliokuwemo katika basi la Happy Nation lililokuwa likitokea Bukoba-Kagera -kwenda Dar es Salaam wamenusurika kifo ,baada ya basi hilo kupinduka upande wa kushoto eneo la Ruvu, Vigwaza , Mkoani Pwani na kusababisha watu nane kujeruhiwa.
Akithibitisha juu ya kutokea kwa ajali hiyo , kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Pwani Pius Lutumo,alisema ,ajali ilitokea Machi 2 saa 8:30 alfajiri,eneo la Ruvu , kata ya Vigwaza Mkoani Pwani, barabara ya Morogoro-Dar es Salaam.
“Bus hilo lenye namba za usajili T.526 DVJ aina ya Zhongton basi mali ya Kampuni ya Happy Nation ikitokea Bukoba-Kagera kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na dereva Vicent Elia Mbasha (39)mkazi wa Mbezi Dar es Salaam liliacha njia na kupinduka wakati akijaribu kukwepa gari lenye namba za usajili T.299 BYF .T 308 aina ya scania:”
Lutumo alieleza ,scania ilikuwa imepata hitilafu na kushindwa kuweka alama za barabarani.
Alitaja majeruhi hao Kuwa ni Selimanda Abdallah (63),Faudhia Ismail(23),Fredina Omary (15),Abtatusi Jovin (18),Nuru Mohammed (38),Idat Remani (27)na Aidan Suleiman (24).
Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge,alifika hospital ya rufaa ya mkoa ya Tumbi,kutoa pole kwa majeruhi na kufafanua, majeruhi walikuwa idadi kubwa lakini walipatiwa huduma kwanza Kituo Cha afya Mlandizi na wengine waliruhisiwa ambapo wengine wamefikishwa hospital ya Tumbi kwa matibabu zaidi.
“Tumefika hospital ya Tumbi ,eneo la emergency room, tumethibitisha hospital yetu imepokea majeruhi hawa hadi sasa waliotokana na ajali hii, Idadi ya majeruhi ilikuwa kubwa ambapo walikimbizwa kituo Cha afya Cha Mlandizi na kupatiwa huduma ,kisha wengine waliruhisiwa kuendelea na shughuli zao nyingine “
Kunenge alitoa rai kwa madereva, kuzingatia sheria za usalama barabarani,kwani dereva wa basi la Happy Nation anadaiwa kufanya uzembe wa kutaka kulipita roli upande wa kushoto na kusababisha kulalia upande huo.
“Madereva waepuke kufanya uzembe ,ambao unaweza kusababisha madhara makubwa , Tunashukuru hakuna kifo kwenye ajali hii,Lakini majeruhi wapo ,wanasababishiwa majeraha ya viungo ambapo kama dereva angefuata sheria yasingetokea haya”alifafanua Kunenge.
Nae mganga mfawidhi hospital ya rufaa ya mkoa ya Tumbi, Amani Malima alieleza ,wamepokea majeruhi sita wa awali wa ajali hiyo na wameambiwa wengine watatu wapo njiani kupelekwa hospitalini hapo.
Alisema kuwa ,majeruhi hao wameumia zaidi maeneo ya mkono,mabega, mgongo lakini wanafanyiwa vipimo vya x-ray na CT-scan ili kupatiwa matibabu endapo watakuwa na madhara yatakayoonekana kitabibu.
“Majeruhi Hawa wa awali wote wameshaanza kupatiwa matibabu,na wanaendelea vizuri, licha ya kwamba watafanyiwa vipimo kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi “alieleza Malima.