……………………
Chama cha ushirika cha Nyanza Bottling Employee (NBE) kimetoa na kukabidhi shuka hamsini zenye thamani ya kiasi cha shilingi laki nane kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya afya ndani ya manispaa ya Ilemela
Akizungumza wakati wa kukabidhi mashuka hayo, Mwenyekiti wa chama hicho Ndugu David Otieno Okumu amesema kuwa sheria ya vyama vya ushirika inavitaka vyama vyote kutenga kiasi kidogo baada ya kupata faida kwaajili ya kuhudumia jamii hivyo kuamua kuchangia msaada huo katika kuimarisha huduma zinazotolewa na Serikali
‘.. Tunapofanya shughuli za maendeleo tunapaswa kuhudumia na jamii inayotuzunguka na sisi tunaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha jamii inapata huduma bora ..’ Alisema
Aidha Bwana Okumu akaongeza kuwa chama chake kimekuwa kikitekeleza takwa hilo la kuhudumia jamii mara kwa mara na kwamba kabla ya kuhudumia Zahanati ya Nyakato walishawahi kufanya hivyo pia katika kituo cha afya Igoma wilaya ya Nyamagana
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni mganga Mkuu wa wilaya hiyo Bwana Charles Samson Marwa amafafanua kuwa Serikali kupitia sera yake ya PPP inaruhusu wadau wengine kushirikiana nayo katika kuhudumia wananchi na kwamba chama hicho cha ushirika kisiishie tu katika kutoa mashuka badala yake kijikite pia katika kuchangia vifaa tiba na kuvifikia vituo vyengine vya kutolea huduma za afya
Nae Afisa ushirika wa manispaa ya Ilemela Bi Theresia Chrisant amesema kuwa chama cha ushirika NBE ni miongoni mwa vyama vikongwe vinavyopatikana ndani ya wilaya yake na kwamba kina wanachama zaidi ya mia nne na hamsini na mtaji wa zaidi ya bilioni nane kikianzishwa tangu mwaka 2001 hivyo kuviomba vyama vyengine kuiga mfano huo
Saguda Ngabi Yohana ni mwakilishi wa mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Mwanza ambapo mbali na kukipongeza chama hicho akaahidi kuvilea na kuvisimamia vyema vyama vyote vya ushirika vilivyomo ndani ya mkoa huo Ili kuhakikisha vinatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotakiwa
Akihitimisha Mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga amekishukuru chama hicho na kuomba kisiishie tu katika Zahanati hiyo badala yake kione namna ya kusaidia na maeneo mengine yenye uhitaji kwani uhitaji ni mkubwa sambamba na kuviasa vyama vingine kuiga mfano huo