Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo wakati
akikagua hatua za utekelezaji wa mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara
ya Mianzini – Olemringa – Ngaramtoni Juu na Olemringaringa – Sambasha –
Timbolo (Km 18) ambao ujenzi wake umefikia asilimia 23, mkoani Arusha. Kushoto
ni Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Steven Zelothe, akiteta jambo na Waziri wa
Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati Waziri huyo akikagua ujenzi wa
barabara ya Mianzini – Olemringa – Ngaramtoni Juu na Olemringaringa – Sambasha
– Timbolo (Km 18) kwa kiwango cha lami mkoani Arusha. Ujenzi wa barabara hiyo
umefikia asilimia 23 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2023.
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Eng.
Reginald Massawe, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof.
Makame Mbarawa pamoja na uongozi wa mkoa wakati wakikagua barabara ya
Mianzini – Olemringa – Ngaramtoni Juu na Olemringaringa – Sambasha – Timbolo
(Km 18) kwa kiwango cha lami ambao ujenzi wake umefikia asilimia 23, mkoani
humo.
Kazi za ujenzi wa barabara ya Mianzini – Olemringa – Ngaramtoni Juu na
Olemringaringa – Sambasha – Timbolo (Km 18) kwa kiwango cha lami zikiendelea
mkoani Arusha. Ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 23 na unatarajiwa
kukamilika mwezi Agosti, 2023.
Serikali imeahidi kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo ya mianzini wanaopitiwa na
ujenzi wa barabara ya Olemringaringa – Ngaramtoni Juu yenye urefu wa kilometa 8.5
inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame
Mbarawa, wakati alipokagua hatua za utekelezaji wa mradi huo wenye jumla ya urefu
wa kilometa 18 unaoanzia Mianzini – Olemringa – Ngaramtoni Juu na Olemringaringa –
Sambasha – Timbolo ambao umefikia asilimia 23 ya utekelezeji wake.
“Sehemu ambazo barabara imefuata wananchi, tutawalipa mara baada ya zoezi la
tathmini linaloendelea kukamilika kwani ni haki yao”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya
Tano, Hayati. Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kujengwa kwa kiwango cha lami na
unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia mia moja na utatekelezwa kwa muda
wa miezi 15 ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti, 2023.
“Serikali hii ni sikivu na inaendelea kutekeleza ahadi zilizotolewa na Serikali za Awamu
zilizopita ili kuendelea kuboresha hali ya miundombinu nchini na kufungua
mawasiliano hususani katika miundombinu ya barabara”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ametoa wito kwa Meneja wa Mkoa wa TANROADS kusimamia ujenzi wa
barabara hiyo na kuhakikisha thamani ya fedha na ubora wa barabara unaonekana pale
ujenzi utakapokamilika.
Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Steven Zelothe, amempongeza Mhe. Rais
wa Awamu ya Sita kwa kuwa wananchi wanaendelea kuona juhudi za dhati
zinazoendelea kufanywa na Serikali hii hasa kwa mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema kuwa
mradi huo utakapokamilika utarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa haraka
wa wakazi wa maeneo hayo na kuongeza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Eng. Reginald
Massawe, ameeleza kuwa barabara hiyo imesanifiwa kubeba ekseli za magari zipatazo
milioni 3 zenye uzito wa tani 8 kila moja katika muda wa miaka 20.
Amesema kuwa hadi sasa mkandarasi amekwishaleta mitambo, vifaa na magari
yanayotumika kwenye kazi za ujenzi wa barabara hiyo na matumaini yao mradi
utakamilika kama ulivyopangwa.
Ujenzi wa wa barabara ya Mianzini – Olemringaringa – Ngaramtoni Juu na
Olemringaringa – Sambasha/Timbolo (Km 18) unatekelezwa na mkandarasi kutoka
kampuni ya STECOL Corporation kutoka China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 22.226.