Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis
akipanda mti katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kilichopo Wilaya ya
Nyamagana jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Soma na Mti” iliyofanyika chuoni
hapo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza, Amina Makilagi akipanda mti katika viwanja
vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kilichopo Wilaya ya Nyamagana mkoani
Mwanza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Soma na Mti” iliyofanyika chuoni jana.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis
na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Amina Makilagi wakishuhudia wanafunzi
kutoka shule ya Awali ya Excelency Academy English Medium ya Nyamagana wakishiriki katika
zoezi la upandaji miti katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jana.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis
akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza mara baada ya kushiriki zoezi la upandaji miti wakati
wa uzinduzi wa Kampeni ya “Soma na Mti” iliyozinduliwa jana.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis
akipata maelezo kuhusu matumizi ya majiko rafiki katika uhifadhi wa mazingira kutoka kwa
Mwakilishi wa Kampuni ya Jiko Janja, Wilson Atukuzwe mara baada ya uzinduzi wa Kampeni
ya “Soma na Mti” iliyozinduliwa katika Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza.
……………………………..
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza
Khamis ametoa rai kwa wizara na taasisi katika sekta za umma na binafsi kutumia
nishati mbadala ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa
Mhe. Khamis amesema hayo Februari 25, 2023 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
‘Soma na Mti’ katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino jijini Mwanza ikiwa ni sehemu
ya kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika taasisi za elimu ya juu
nchini.
Amesema zoezi la upandaji katika maeneo mbalimbali nchini ni ajenda ya kitaifa
inayoongozwa na viongozi wa kitaifa akiwemo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais Mhe.Dkt Philip Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na
hivyo kuzitaka taasisi za umma na binafsi kuunga mkono juhudi hizo.
“Tupo hapa kutekeleza mpango wa Serikali juu ya utunzaji wa mazingira ikiwa ni
muendelezo wa juhudi zilizoanzishwa na viongozi wetu wakuu wa kitaifa. Nitoe rai kwa
viongozi wa ngazi zote kuhakikisha tunasimamia maelekezo ya Serikali ya kuzuia
ukataji miti, tuanze kutumia nishati mbadala kama gesi kwa ajili ya kupikia kama
anavyosisitiza Rais wetu,” amesema Mhe. Khamis
Aidha naibu waziri huyo ametoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini
kuhakikisha kuwa wanasimamia na kuendeleza kampeni hiyo kwa kuhakikisha kila
shule na kila mwanafunzi anakuwa na mti wake na kuhimiza utamaduni wa kila Kaya
kupanda miti na kila mtu anayenunua eneo kuhakikisha amepanda miti katika eneo
lake.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi amesema
suala mazingira ni moja ya kipaumbele vya msingi kinachotekelezwa na taasisi zote za
umma na binafsi zilizopo katika Wilaya hiyo na kukusudia kulifanya Jiji la Mwanza
kuendelea kuwa Jiji la kijani.
“Katika Wilaya ya Nyamagana kila mradi unaotekelezwa unafungamanishwa na
mazingira na kila tukio tunapanda miti na hivi karibuni taasisi zetu za TFS, Gereza la
Butimba na wadau wengine tulipanda zaidi ya miti 7000 katika vyanzo mbalimbali vya
maji ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Makamu wa Rais,” amesisitiza Makilagi.
Ameongeza kuwa kupitia kampeni ya “Soma na Mti” wilaya hiyo imejipanga kimkakati
katika kuhakikisha kuwa inafikia lengo la kupanda miti 1,500,000 kwa kushirikisha shule
za msingi, sekondari na taasisi za elimu ya juu na kuhakikisha inarejesha hadhi ya Jiji la
Mwanza kuwa kinara wa usafi wa mazingira nchini.
Naye Balozi wa Mazingira Nestory Mushi amesema kupitia taasisi yake ya Mweka Site
wamefanikiwa kuotesha miti zaidi ya 358,000 na miti hiyo inatarajia kupandwa katika
Mikoa yote inayokabiliwa na hali ya ukame.
Taasisi yetu inahamisha jamii katika shughuli zote za usafi wa mazingira ikiwemo
upandaji miti na usafi wa fukwe mbalimbali. Tunafundisha wanafunzi wa ngazi
mbalimbali ikiwemo shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuhusu vitalu vya miti,
miradi ya samaki na utunzaji mazingira” amesema Mushi.
Mwakilishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Alex Julius amesema
katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuhamasisha utunzaji wa mazingira ikiwemo
upandaji, TFS imeanzisha kitalu cha miti ya matunda na vivuli ambapo kati ya Julai
2022 hadi Februari 2023, TFS imefanikiwa kuzalisha miche ya miti 67,310.
Wakati wa kuzalisha miche hii tunazingatia masuala mbalimbali ikiwemo miche
inayokuwa haraka, miche inayohifandhi maji, miche inayozuia mmomonyoko wa
udongo na kuanzia mwezi Julai 2022 hadi Februari 2023 miche ya miti 32,970
imegawiwa bure katika taasisi mbalimbali” amesema Julius.
Kampeni ya “Soma na Mti” ilizindiliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2022 ikiwa
imelenga kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuona
zoezi la upandaji miti kuwa sehemu muhimu ya maisha ili kukabiliana na changamoto
za mabadiliko ya tabianchi.