Mgeni rasmi katika Mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari Coastal, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona (katikati) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi, Gabriel Habashi (kushoto) na kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Gasper wakati wa mahafali hayo jijini Tanga jana.
Mgeni rasmi katika Mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari Coastal, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona akigawa vyeti kwa wahitimu wa shule hiyo katika mahafali yaliyofanyika jijini Tanga jana.
Mgeni rasmi katika Mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari Coastal, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika jijini Tanga jana.
…………………………….
Katika kampeni yake ya kuhamasisha kilimo cha Mkonge nchini, Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), iko kwenye mchakato wa kuanzisha klabu za wanafunzi katika shule za sekondari kwa lengo kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia kilimo hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema hayo jana katika mahafali ya Kidato cha Sita ya Shule ya Sekondari Coastal jijini Tanga ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Pamoja na mambo mengine amesema kwa kuanza na klabu hizo wataanza na shule hiyo kwa majaribio kabla ya kuhusisha shule nyingine huku akiahidi kulifanyia kazi ombi la uongozi wa shule hiyo kuwapatia ardhi kwa ajili ya kulima Mkonge.
“Kama mnavyofahamu Bodi ya Mkonge ni taasisi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ni kama imekufa sasa tumekuja kama kuifungua rasmi ofisi kama jengo na sekta ya Mkonge kwa ujumla wake.
“Lakini tunategemea tunapokwenda mbele vijana wengi sana kutoka kwenye shule za Tanga ndiyo wahusike kwenye mpango mzima wa kuleta mapinduzi kwenye zao la Mkonge kwani sasa hivi tunapozungumzia mkonge tunazungumzia bidhaa moja tu ya nyuzi za mkonge zitengeneze vikapu, makapeti, magunia, kamba na bidhaa nyingine zitokanazo na Mkonge,” alisema.
Mkurugenzi Kambona alisema Mkonge ni zao ambalo mnyororo wake wa thamani una shughuli nyingi sana ambazo zinaweza zikafanywa kwa vijana ambapo kama tafiti zitafanyika vizuri zitazalisha ajira nyingi.
“Tunapokwenda mbele tunataka ikiwezekana tufungue klabu kwenye shule ya zao la Mkonge, ile mipango ya kuhusisha wanafunzi kwenye vile vitalu vya kuwajenga vijana kwa ajili ya kuendeleza zao la Mkonge itaanza kwa kuihusisha Shule ya Coastal.
“Bodi ya Mkonge pia tunafikiria tuwe na miradi ya wanafunzi ambayo tutaifadhili, watafanya tafiti mbalimbali kwenye zao la Mkonge kuangalia mabaki ya Mkonge kama sasa hivi tunaambiwa kwamba kwenye Mkonge unaweza ukapata ethanol, unaweza ukatengeneza pombe ya tequila, sukari ya mkonge, kuzalisha uyoga na mengine,” alisema.
Alisema Serikali ya Tanzania imepitia katika hatua mbalimbali za kielimu tangu tupate uhuru na kila hatua imelenga katika lengo la kumfanya mhitimu wa masomo fulani kuwa na ujuzi utakaomwezesha kuyatawala mazingira yake
“Sasa hivi kuna tatizo kubwa la ajira kuna vijana wengi wamesoma ngazi za chuo kikuu lakini hawana kazi mtaani ambao wamesoma lakini hawana ajira mbaya zaidi ni kuwaona vijana hao wakiwa wamekaa tu bila kujishughulisha na hapo ndiyo utajiuliza je elimu yao imewasaidia nini kama vijana hawa hawawezi kujiajiri hata kidogo.
“Hivyo nawaasa wahitimu mnapoingia mtaani msibweteke, jitahidini kujishughulisha na mambo mbalimbali yatakayowaingizia kipato ikiwezekana mje Bodi ya Mkonge tuwapatie mashamba,” alisema
Kuhusu ombi uongozi kwamba Bodi inaweza kuangalia namna gani itaisaidia shule hiyo kuipatia ardhi kama shule ikiwa sehemu ya kuiongezea mapato alisema Bodi itajitahidi kuhakikisha inawapatia ardhi isiyopungua ekari 100.
“Bodi itajitahidi kutekeleza hilo pamoja na kuwapatia masuala ya ushauri wa kiufundi wa namna gani mnaweza mkaanza kilimo cha Mkonge na wataalamu wangu wa TSB watajihusisha moja kwa moja na uongozi wa shule kuhakikisha tunaanza jambo hili.
“Tuna maombi mengi yanayosubiri bado ya taasisi mbalimbali hatujayasahau hayo maombi tunatumaini yatakwenda sambamba na maombi haya ya shule,” alisema.
Awali, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Gasper alisema kutokana na changamoto ya kusuasua kwa malipo ya ada kutokana na changamoto za kiuchumi na kijamii lakini kubwa zaidi ni shule kutegemea chanzo kimoja cha fedha ambacho ni ada ambapo alimuomba Mkurugenzi Kambona kuwapatia ardhi kwa ajili ya kulima Mkonge kama chanzo mbadala cha fedha.
“Lakini pia tungependa kuanzisha uhusiano na taasisi mbalimbali ikiwamo Bodi ya Mkonge ikiwezekana kufungua klabu zinazoendana na malengo yao lakini pia kutumia shule na wanafunzi kama mabalozi wa bidhaa mfano kutangaza zao la Mkonge.
“Tukiwa wadau wa Mkonge, mwaka huu shule iliandaa Makala maalumu ya utunzaji wa mazingira na kuhamasisha utalii inayoitwa ‘Urithi wa Pwani’ ambapo vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani Tanga ikiwamo zao la Mkonge vimetangazwa na washiriki wakuu walikuwa wanafunzi wetu wa Klabu ya Mazingira na Utalii ambao wengi ni kidato cha sita,” alisema.