Muogeleaji Lina Goyayi akichapa maji katika mashindano yaliyopita
Muogeleaji Terry Tarimo akipambana katika mashindano yaliyopita.
………………..
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Klabu 13 zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya kuogelea ya Taliss-IST yaliyopangwa kufanyika Februari 25 na 26 kwenye Bwawa la Kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Masaki.
Meneja wa klabu ya Taliss-IST, Hadija Shebe amezitaja klabu hizo kuwa Dar es Salaam Swim Club (DSC), Bluefin, Morogoro Piranhas, Mwanza Swim Club, Wahoo Zanzibar, FK Blue Marlins na klabu kutoka Uganda Flash Swim Club.
Klabu nyingine ni Braeburn Arusha, Premiere Swim Club (Dar es Salaam), Mwanza Swim Club, Lake Swim Club, Taliss-IST na HPT.
Hadija alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika na waogeleaji wanafanya mazoezi ili kushindania zawadi mbalimbali siku hiyo.
Alisema kuwa waogeleaji zaidi ya 200 wanatarajia kushiriki katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na International School of Tanganyika (IST), Bwana Sukari, Pepsi, Jubilee Insurance, Dehli Darbaar, Wrap and Roll, F and L Juices na Burgers 53.
Kwa mujibu wa Hadija, waogeleaji watashindana katika umri tofauti katika staili mbalimbali kwa mujibu wa taratibu. Alisema kuwa kutakuwa na kundi la waogeleaji chini ya miaka 8, 9 na 10, 11 na 12, 13 na 14, na zaidi ya miaka 15.
Alisema kuwa mbali ya staili tano za kuogelea, waogeleaji hao watashindania katika relei ambayo kwa mtindo wa Individual Medley (IM) na Freestyle. Kwenye IM, waogeaji watachanganya staili nne ambazo ni butterfly, backstroke, breaststroke, na freestyle.
“Waogeleaji watakaoshinda katika mashindano hayo watazawadiwa medali na vikombe, tunawaomba wadhamini wajitokeze ili kufanikisha mashindano haya ambayo ni maarufu na yenye mvuto mkubwa,” alisema Hadija.