Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo hadi kufika Februari Mwaka huu
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA), Matilda Kasanga akiongoza kikao baina ya Waandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Dkt. Stephan Ngailo.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo tofauti wakifuatilia mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo
………………………..
Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuwainua wakulima kupitia uimarishaji na utoaji wa elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea ili waweze kuzalisha kwa faida na tija kubwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo amesema kuwa Serikali kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 ilitoa fedha ili kugharamia mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini.
“Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 150 kugharamia ruzuku ya mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 iliyotolewa kwa wakulima wote nchini na hadi kufikia mwezi Februari 2023, TFRA imesajili waingizaji wa mbolea 28, wazalishaji 3 ambao wanashiriki kuingiza, kuzalisha na kusambaza mbolea ya ruzuku msimu wa 2022/2023 kwa wakulima wote nchini”, Alisema Dkt. Ngailo.
Dkt. Ngailo amesema, TFRA imesajili mawakala 3,428 wanaosambaza na kuuza mbolea ya ruzuku katika mikoa 26 nchini na kufikia Februari 2023, wakulima 2,916,703 walikuwa wamesajiliwa kwenye mfumo wa kupata namba maalum ya kununulia mbolea hiyo ambayo itapunguza gharama za uzalishaji na kutoa tija kwa wakulima nchini.
Aidha, kufuatia Serikali kusisitiza matumizi bora ya mbolea kwa wakulima, ongezeko la matumizi ya mbolea nchini ni kubwa kwa wakulima ambapo Nyanda za Juu Kusini inaongoza kwa usajili wa wakulima 1,209,692, Kanda ya Kati wakulima 501,941, Kanda ya Ziwa wakulima 488,845 Kanda ya Kaskazini wakulima 423,921 na Kanda ya Mashariki wakulima 289,218.
Aliongeza kuwa Bei ya mbolea zilizoko katika mfumo wa Ruzuku ni shilingi 50,000 hadi 70,000 kwa mbolea inayoingizwa kutoka nje ya nchi na shilingi 60,000 hadi 70,000 kwa mbolea inayozalishwa ndani ya nchi, hadi Februari 2023 jumla ya tani 290,200.525 zimeuzwa kwa jumla ya wakulima 710,021, pia tani 54,061 zimeuzwa nje ya mfumo wa mbolea ya ruzuku.
“Kuhusu utoaji wa Mafunzo mpaka Sasa TFRA imetoa Mafunzo,kusajili Kwa mujibu wa kifungu Cha 4(1) cha Sheria ya Mbolea,2009 na kuwatangaza katika Gazeti la Serikali wakaguzi wa Mbolea 140 waliopo TFRA na Halmashauri za Wilaya,Mamlaka imetoa Mafunzo Kwa maafisa Kilimo 59 wa Halmashauri na Mikoa ambao taratibu za kutangazwa Kwenye gazeti la Serikali zinaendelea”amesema Dkt Ngailo
Dkt Ngailo amesema kuwa TFRA tangu kuanzishwa kwake imepata mafanikio mbalimbali katika tasnia hiyo Kwa uchumi wa Nchi ikiwa ni pamoja na kudhibiti ubora wa Mbolea,lakini pia imeweza kusajili jumla ya Mbolea 481 mpaka kufika Februari Mwaka huu.