Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha ,Mussa Ndomba amesema,katika Mpango wa bajeti ya 2023/2024 jumla ya shule za Sekondari tatu na moja shule ya Msingi zitajengwa.
Baraza la madiwani lililoketi , Jumatano Februari 22,2023 kupitia na kuridhia mapendekezo ya bajeti kwa Mwaka wa fedha 2023/2024, limebariki shule hizo zitajengwa kwenye Kata ya Mkuza shule moja ya sekondari,Kata ya Tangini shule moja ya Sekondari na Kata ya Kibaha zikijengwa shule mbili Msingi na sekondari ili kuwaondolea kero wanafunzi .
Vilevile alieleza, huduma za afya katika Halmashauri hiyo zimeendelea kutazamwa na Sasa jumla ya Milioni 641,763,000 zimetengwa kuiboresha zaidi Idara ya Afya.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya uchumi na huduma za jamii ,Kambi Legeza alieleza,Halmashauri ya Mji Kibaha itaendelea kuboresha huduma za afya .
“Kiasi cha Sh.milioni 641,763,000 kimetengwa kuboresha na kuimarisha huduma za afya ambapo kiasi cha milioni 300,000,000 kitatumika kununua Vifaa tiba na vitendanishi kwa ajili ya hospitali ya Wilaya na Zahanati huku Milioni 50,000,000 ikitumika kukamilisha ujenzi wa zahanati na Milioni 411,763,000 zikitumika kutoa chanjo na Huduma nyingine za kitabibu.
Pamoja hayo , Halmashauri hiyo imejipanga kujenga Hotel ya Kisasa ili kupanua wigo wa Mapato yake ya ndani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha alisema utanuaji wa vyanzo vingine vya Mapato unalenga kwenda kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Selina Msenga alisema Mapato ya ndani ndiyo yatakayotumika kujenga hotel na Miradi mingine hivyo alitoa rai kwa Vibarua wanaopata ajira za kukusanya Mapato ya Halmashauri kuacha tabia ya udokozi kwani tabia hiyo ni kufifisha juhudi zinazofanyika.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tumbi ,Raymondi Chokala na Goodluck Manyama wa Kata ya Kibaha walisisitiza kutelezwa kwa bajeti kama ilivyopangwa ili kufikia malengo.
Mfalme Kabuga ambae ni Diwani wa Kata ya Tangini amekuwa akipambana kupata Zahanati kwenye Kata yake na Sasa bajeti hii inakwenda kutatua kilio cha wananchi wake hivyo ametumia fursa hiyo kuwapongeza wataalam kwa bajeti nzuri.