Na Mwandamizi wetu, Manyara
MWENYEKITI wa chama cha wafanyakazi wa vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA) Mussa Juma amesema itakuwa nafuu kwa waandishi wa habari baada ya muswada wa huduma za habari kuwasilishwa Bungeni.
Juma akizungumza juu ya hilo amesema uhuru wa waandishi wa habari kuandika habari zao kwa uhuru zaidi utafikia hatua nzuri pindi wabunge wakipitisha baada ya kuwasilishwa Bungeni.
“Muswada wa huduma za habari namba 12 wa mwaka 2016 baada ya kuwasilishwa Bungeni ni hatua nzuri kwani utachangia kufanikisha uhuru wa habari,” amesema Juma.
Amesema waandishi wa habari nchini watakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya kazi zao mara baada ya muswada huo kupitishwa na Bunge kuwa sheria rasmi.
Amesema baada ya kupitishwa Bungeni itakuwa nafuu kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao ipasavyo hususani kuandika habari za uchunguzi.