Menejimenti ya Tume ya Ushindani nchini ( FCC) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bw. William Erio, imetembelea Bandari ya Tanga kwa lengo la kujionea utendaji wake huku ikiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kukabiliana na suala la uingizaji wa bidhaa bandia.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo akiwa Bandarini hapo, Bw. Erio pamoja na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika katika kutekeleza miradi mikubwa itakayoinua, kukuza uchumi wa Nchi na kuleta maendeleo kwa watanzania ikiwa ni pamoja na upanuzi wa bandari ya Tanga unaoendelea kufanyika sasa, alisisitiza kuwa FCC kulingana na utekelezaji wa majukumu yake kisheria ya udhibiti wa bidhaa bandia imejipanga kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kuendana na maboresho hayo.
“Tumeambiwa kuwa mara upanuzi huu utakapokamilika utaifanya bandari hii kuweza kupokea mizigo zaidi ya tani Milioni 3 kwa mwaka kutoka tani 700,000 za sasa, hivyo FCC tuna wajibu wa kuisaidia Serikali na tutahakikisha tunajiweka sawa na kuwa mahali hapa wakati wote kutoa huduma inavyostahiki” alisema Bw. Erio.
Aidha, alisema kuwa FCC kama taasisi iliyopewa jukumu la kusimia suala la udhibiti wa bidhaa bandia nchini, watafanya kazi bega kwa bega kwa mujibu wa Sheria na kushirikiana kikamilifu na watendaji wa bandari hiyo ili kuhakikisha malengo ya Serikali kupitia bandari hiyo yanafanikiwa hivyo kuisaidia Serikali kutimiza kusudio lake la upanuzi huo sambamba na ukuzaji wa biashara na uchumi nchini.
Alisema bandari hiyo mbali na kutumiwa kwa ajili ya mizigo ya hapa nchini, pia inatumiwa na nchi jirani kuingiza mizigo yao, hivyo wao kama mojawapo ya taasisi zilizopewa dhamana na Serikali wana kila sababu ya kuwa sehemu ya taasisi nyingine mahali hapo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na bandari hiyo zinakuwa zenye ufanisi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa udhibiti wa bidhaa bandia nchini kutoka FCC, Bi. Khadija Juma Ngasongwa, allisema katika kuunga mkono juhudi za Serikali zinazoendana na upanuzi wa bandari hiyo na kusisitiza kuwa kwa upande wao katika Kurugenzi ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia wamejiimarisha kuhakikisha wanadhibiti uingizaji wa bidhaa zote bandia zitakazoingizwa kupitia bandari hiyo.
Alisema ziara yao hiyo katika bandari ya Tanga imekuwa chachu kwa FCC pamoja na watendaji wake kwakuwa itawawezesha kuendelea kujipanga zaidi katika kudhibiti bidhaa bandia zinazoingizwa nchini kwa lengo la kumlinda mtumiaji.