Wadau mbalimbali wamechangia maoni yao kuhusu muswada wa habari baada ya kusoma bungeni kwa mara ya kwanza kuwa wanatarajia kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari ambapo zitaweza kufanya kazi zao uhuru zaidi .
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Naibu katibu Mkuu BAWACHA BARA,Nuru Ndosi wakati akitoa maoni yake ofisini kwake kuhusiana na muswada huo.
Amesema kuwa ,muswada huo unaweza kutoa chachu kubwa kwa wanahabari na hata vyombo vya habari kuweza kuripoti habari mbalimbali zenye kusaidia jamii na kuripoti habari hizo bila kuwepo kwa vizuizi vyovyote.
“Unajua baada ya kusomwa kwa muswada huu wa habari ni matarajio ya kila mmoja kuona mabadiliko makubwa katika vyombo vya habari ikiwemo kuwepo kwa uhuru wa kutosha katika kuripoti habari mbalimbali na kufichua maovu mbalimbali katika jamii kwani kuna mambo mengi sana ambayo yamekuwa yakitokea kwenye jamii na hayaripotiwi ila kupitia muswada huo kutakuwepo na uhuru wa kuripoti maswala hayo”amesema Ndosi.
Aidha amevitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kufichua maovu katika jamii na kuibua changamoto mbalimbali baada ya kupitishwa kwa mswada huo kwani wanakuwa na uhuru mkubwa wa kuripoti na kusaidia jamii kwa kiwango kikubwa sana.