………………..
WASANII wametakiwa kujielekeza katika utungaji wa nyimbo zenye mashairi kuhusu maendeleo yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan sambamba na zile zinazolenga kuielimisha jamii juu ya mambo mbalimbali yailiyopo katika mazingira wanayoishi.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT)Mkoa wa Njombe Scholastica Kevela wakati wa uzinduzi wa Albamu ya kwanza ya Msanii wa nyimbo za Bongfleva Avo Star(Keisal) anayetokea mkoani Njombe.
Katika hafla hiyo iliyofanyika mkoani humo na kuudhuriwa na Mbunge wa Lupembe Edwin Swale, baadhi ya wenyeviti na makatibu wa jumuiya za CCM Mkoa huo pamoja na madiwani kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Nombe.
Kevela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu hiyo iitwayo ‘Last Chance’ amesema wasanii wote wakiwemo wa mkoa huo kupitia sanaa yao wanayo nafasi kubwa ya kutangaza mambo mazuri yanayofanywa kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuiletea maendeleo Tanzania.
“Tunatambua mchango mkubwa mnaoutoa katika sanaa ndani ya Taifa letu, ombi langu kwenu tumieni nafasi yenu ya sanaa kuimba nyimbo zinazozungumzia mambo mazuri yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya Taifa hili” amesema Kevela
Pamoja na hilo Mwenyekiti huyo piano alitoa rai kwa wasanii wa Mkoa huo kusajili kazi zao Basata ili ziweze kutambulika sambamba kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Baraza hilo ili ziweze kuwasaidia katika kazi zao za sanaa.
Aidha Kevela alimpongeza msanii Avo Star kwa uthubutu aliounyesha kutoa albamu hiyo na kumweleza kuwa ameitendea haki nafasi ya ufadhili wa masomo katika chuo cha Sanaa Bagamoyo aliyoipewa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akimchangia kiasi cha Sh Milioni 1 kati ya Sita ambazo Msanii huyo alikusudia kuzikusanya katika hafla hiyo iliyofanikisha kukusanya zaidi ya Milioni 4 kutokana na harambee iliyoongozwa na Mwenyekiti huyo.
Mbali na hilo pia amewapongeza wadau wote wakiwemo viongozi wa chama na Serikali wa Mkoa huo kwa ushirikiano wao na kujitoa kwao katika kumuwezesha Msanii huo ba wengine waliopo katika mkoa huo.
Kwa upande wake Mbunge wa Lupembe Edwin Swale pamoja na kumpongeza Avo Star kwa kufanikisha ujio wa albamu yake hiyo ya kwanza, aliwataka wasanii wa mkoa huo kushikana mikono na kuonyesha mshikamano katika shughuli zao za kisanaa ili kuutangaza mkoa huo.
Naye Msanii Avo Star ameshukuru Mgeni Rasmi wa hafla hiyo(Scholastika Kevela) kwa moyo wake uliowezesha kukusanya fedha hizo alizoahidi kuwa atazitumia katika kuendeleza kazi zake za kisanaa.