Imeelezwa kwamba, mfumo unaotumika kusambaza mbolea za ruzuku umesaidia kuondoa biashara haramu ( black market) ya mbolea na kupunguza ushindani kwenye soko la ndani kufuatia bei ya bidhaa hiyo kwa wakulima kuwa ni moja nchi nzima.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mauzo wa kampuni la mbolea la Mohamed Enterprise Kanda ya Kaskazini, Jafar Abbas alipokuwa akizungumza na wanahabari waliofika lilipo ghala la mbolea ya kampuni hiyo Jijini Arusha.
“Mfumo umeondoa biashara ya magendo na tabia za watu kuhodhi mbolea ili baadaye wauze kwa bei ya juu” Abbas anasisitiza.
Amesema, mfumo huo pia umewasaidia wafanyabiashara na serikali kwa ujumla kupata takwimu sahihi za kiasi cha mbolea kilichouzwa kwa wakulima na kiasi kilichopo kwa ajili ya usambazaji.
Aidha, Abbas ameeleza kuwa, mfumo wa mbolea ya ruzuku umewasaidia wakulima kununua bidhaa hiyo kwa bei halali tofauti na awali ambapo kila mfanyabiashara aliuza bei yake ilimradi alizingatia bei elekezi iliyotolewa na serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, (TFRA).
Kwa upande wake Richard Kika Afisa Masoko wa Mohamed Interprise tawi la Arusha amesema awali kampuni lao lilikuwa likiuza mbolea Jijini Dar es Salaam na wamefungua matawi mengine hususani la Arusha Mwezi September, 2022.
Aliongeza kuwa, kiasi cha mbolea kilichouzwa mpaka mwishoni mwa mwezi Januari, 2023 ni tani 782 ambapo msimu wa kilimo mkoani humo bado haujaanza na kubakiwa na mifuko 623 ya mbolea ghalani huku wakitarajia kuongeza mauzo kutokana na mwitikio wa wakulima wa kutumia mbolea msimu huu wa kilimo.
Ameeleza kuwa, bado mbolea nyingine inaendelea kuletwa ili kukidhi mahitaji ya wakulima kwa msimu wa kilimo unaoanza mwezi Februari kwa mikoa ya Kaskazini.