OkJukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeomba kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kusaidia ili Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) uweze kufikishwa bungeni na kufanyiwa kazi na waheshimiwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunamuomba Mh.Rais Samia Suluhu Hassan anusuru hali hii katika suala la mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016).Tunaomba tukutane na Mhe. Rais Samia, tukiamini mkutano huo utatukwamua tulipokwama.
Hii inatokana na ratiba ya vikao vya bunge kuonesha kwamba Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) hautasomwa katika bunge hili jambo ambalo linaonekana kutakuwa na mkwamo wa marekebisho hayo ya sheria ya habari ambayo kwetu ni muhimu sana.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF leo imesema jukwaa hilo limekuwa na mawasiliano mazuri na Waziri Nape; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dk. Eliezer Feleshi; Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali, Onorius Njole; na Ofisi ya Bunge.
“Mwanzo tuliahidiwa muswada wa mabadiliko ungeingizwa bungeni mwaka 2022 katika vikao vya
Februari, wakasema Aprili, baadaye Septemba, ikasogezwa Novemba, lakini kote huko hakuna kilichotekelezwa”
“Suala la kubadili sheria hii limekaa muda mrefu na sisi tunapodai Uhuru wa Habari si kwa sababu ya wanahabari pekee, hapana. Uhuru huu ni wa Watanzania wote kutoa maoni yao; na kwa kufanya hivyo tunakuza demokrasia nchini na kuongeza uwajibikaji kwa watu wote nchini” imesema Taarifa hiyo.
Jukwaa la Wahariri na Wadau, kwa kuona kazi kubwa anayoifanya Rais Samia ya kurejesha uhuru
katika sehemu mbalimbali nchini ikiwamo kufungulia magazeti ya Mwanahalisi, Mseto, Tanzania
Daima na Mawio, kurejesha Bunge Live, kushusha bei za leseni za TV na Radio, iliamini njia ya diplomasia ingeiwafikisha katika nchi ya ahadi lakini inaonesha bado kuna mkwamo.