Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Edward Mjema amesema ni lazima Viongozi wote nchini wasikilize kero na kuzitatua kwa haraka na muda mfupi sana badala ya kurundikana kwa kero na migogoro mingi inayochukua muda mrefu.
Mjema ameyasema hayo akiwa kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel iliyoanza leo Jumamosi mkoani Morogoro kwa kuanzia wilaya ya Gairo.
“Viongozi wote tuliopo tuhakikishe tunasikiliza kero kwa karibu sana. Hizi kero zikisikilizwa kuanzia chini haiwezi kuleta mrundikano wa kero kwenye ngazi za juu za Viongozi. Lazima tusikilize kero na kero unaposikiliza ni lazima iishe siku ileile au katika wiki kero iwe imefungwa.” Alisema Mjema akitoa ujumbe kwa Viongozi wote.
Mjema aliendelea kusema kwamba haileti afya kwa kero ileile kuendelea kuwepo kila siku kwasababu kero nyingi zinazotokea hata kwenye mashamba na migogoro ya wakulima na wafugaji zinafahamika na watu wanajuana hivyo ni lazima kuanzia chini zisikilizwe na kumalizwa huku akiwasisitiza Viongozi kuwa karibu katika kusikiliza na kumaliza kero.
Katika hatua nyingine, Mwenezi Mjema ameendelea kuwasisitiza Wana CCM kote nchini kuendelea kuimarisha Chama kwa kukitangaza zaidi kupitia shughuli kubwa inazofanya kwa wananchi ili kiendelee kuwa imara kushika dola na kazi hii ya kukitangaza na kukiimarisha Chama ianze kuanzia ngazi ya chini ya Kitongoji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na Taifa.