Mratibu wa Mradi wa ALIVE – Tanzania kutoka Shirika la Milele Zanzibar Foundation, Bw. Samson Sitta (katikati) akizungumza na wanahabari leo kuzungumzia uzinduzi wa tathmini ya utafiti wa ALiVE uliofanyika katika wilaya 34 ndani ya mikoa 18 ya Tanzania Bara, uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Januari 26, 2023 jijini Dar es Salaam Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Kulia ni Mtafiti Kutoka UDSM, Daniel Marandu pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Uwezo Tanzania, Bw. Benjamin Masebo (kushoto) wakifuatilia. |
Na Mwandishi Wetu
UTAFITI uliofanywa na Mradi wa ALiVE-Tanzania kupima stadi za maisha na maadili kwa vijana nchini Tanzania umebaini kuwa vijana wengi wenye umri kati ya miaka 13 – 17, wana kiwango cha chini cha stadi za maisha (LifeSkills). Imebainika kuwa kundi hilo la vijana linauwezo mdogo wa utambuzi wa matatizo na hata kutumia namna bora ya kulitatua kwa jamii.
Matokeo ya kina ya utafiti huo uliofanywa ndani ya Wilaya 34 kutoka katika mikoa 18 ya Tanzania yanatarajiwa kuzinduliwa Januari 26, 2023 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Mradi wa ALIVE – Tanzania kutoka Shirika la Milele Zanzibar Foundation, Bw. Samson Sitta anasema tathmini ya utafiti wa ALiVE imefanyika katika wilaya 34 ndani ya mikoa 18 ya Tanzania Bara, kati ya mwezi Juni hadi Septemba 2022, huku akishirikisha jumla ya vijana 14,645 wenye umri wa miaka 13-17 walifanyiwa tathmini/upimaji kutoka katika kaya 11,802.
Akifafanua zaidi juu ya utafiti huo alisema umebaini ni asilimia 8 tu ya vijana wana uwezo wa utatuzi wa matatizo, yaani, wanaweza kutambua kuwepo kwa tatizo kutoka kwa mitazamo tofauti tofauti, wakielewa kuwa kunaweza kuwa na njia nyingi na kuchagua iliyobora.
“Kwa kutilia mkazo, stadi za maisha na tunu zinatambuliwa kuwa ni sehemu ya msingi ya elimu kwani huongeza uwezo wa kujifunza kwa wanafunzi. Pia kwa upande wa ajira, waajiri nao wanazingatia zaidi umahiri wa stadi za maisha na maadili kama vile utatuzi wa matatizo, ubunifu, mawasiliano, fikra tunduizi, ushirikiano, kujitambua na stadi nyinginezo ili kuongeza ufanisi katika kazi,” alisema Bw. Sitta.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uwezo Tanzania, Bw. Benjamin Masebo aliongeza kuwa licha ya ukweli kwamba watu wengi wanakubaliana kwamba stadi za maisha ni muhimu, hakuna ushahidi wa kutosha unaotoa taswira ya kiwango cha umahiri wa watoto katika stadi za maisha na maadili, zaidi ya matokeo ya kitaaluma.
“Sasa tumeweza kufanya kwa mara ya kwanza tathmini ya kitaifa ya stadi za maisha na maadili kwa vijana na kupata matokeo. Hivyo basi baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo, ni wakati maridhawa kujikita katika mijadala chanya kuhusu nini tutaweza kufanya ili kuwajenga watoto wa Tanzania katika stadi hizi kupitia mfumo wa elimu na malezi nyumbani.
“Tunatarajia ripoti hii ya kipee kabisa kuwahi kutolewa Tanzania, na Afrika Mashariki, itachochea mijadala chanya kuhusu umuhimu wa stadi za maisha na nini kifanyike kuhusu ujifunzaji wa watoto wetu ili kuwasaidia kujenga stadi hizi.” alifafanua Kaimu Mkurugenzi wa Uwezo Tanzania, Bw. Masebo.
ALiVE ipo chini ya Mtandao wa Kikanda wa Elimu na Ujifunzaji (Regional Education Learning Initiatives-RELI), kupitia kongani ya maadili na stadi za maisha (VALi) hii inaratibiwa na Zizi Afrique Foundation NGO iliyoko nchini Kenya, Luigi Giussani Taasisi ya Elimu ya Juu nchini Uganda na Milele Zanzibar Foundation kwa Tanzania.
Tathmini ya ALiVE kwa Tanzania bara ilifanywa kwa Ushirikiano wa mashirika mawili; Milele Zanzibar Foundation na Uwezo Tanzania.