……………….
Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji Dar es salaam wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wakiwa na samaki KG 980 zilizokuwa ndani ya boti yenye usajili nambari Z. 103585 jina MV MAEDRA.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji (T) Dar es Salaam ACP Moshi Sokoro amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo mnamo 12/01/2023 majira ya asubuhi huko maeneo ya soko la Samaki Ferry wakiwa katika operesheni ya pamoja ya kuzuia uvuvi haramu na makosa mengine ya kijinai walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
Aidha amesema samaki hao wanasadikika kuvuliwa kwa kutumia Baruti. Taratibu za kuwafikisha watuhumiwa mahakamani zinaendelea.
Jeshi la Polisi limewapongeza wananchi wote ambao wanachukia uhalifu na limewaomba waendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wahalifu hao.
Pia Jeshi hilo limetoa onyo kwamba halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayejihusisha na uvuvi haramu pamoja na makosa mengine ya kijinai