Na. Edmund Salaho/SERENGETI
Spika wa Bunge la India, Mhe. Om Birla ametembea Hifadhi ya Taifa Serengeti ikiwa ni sehemu ya mapumziko pamoja na kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika Hifadhi hii.
Akizungumza baada ya mapokezi hayo Naibu Kamshna wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Magharibi TANAPA, Martin Loibooki alisema
“Tunajivunia na kuona fahari kwani Spika wa Bunge la India ni mtu maarufu nani kiongozi mkubwa nchini kwao, ujio wake katika Hifadhi ya Taifa Serengeti utasaidia kuendelea kuitangaza Hifadhi hii na kufanya wageni wengine mashuhuri kutembelea lakini pia watalii kutoka Taifa la India ambalo Mhe. Om Birla anatoka”
Upendo Massawe, ambaye ni Afisa Mhifadhi Mkuu na Msimamizi wa Idara ya Utalii, Serengeti amebainisha kwamba Hifadhi ya Taifa Serengeti imejidhatiti vilivyo kuhakikisha wageni wote wanaotembelea hifadhini wanafaidi uzuri wa vivutio vyote vinavyopatikana katika hifadhi hii.
Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo ni ya kwanza kuanzishwa nchini Tanzania ni maarufu zaidi ulimwenguni na imekuwa ikitembelewa na wageni mashuhuri kutokana uwepo wa matukio ya uhamaji wa Nyumbu maarufu kama“WILDEBEEST MIGRATION” ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii hifadhi hapo na hivyo kuifanya Serengeti kwa mara nne mfululizo kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika maarufu kama
“WORLD TRAVEL AWARDS”.