Eng. Christopher Kalist akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alipokagua ujenzi wa reli ya kisasa SGR
sehemu ya Isaka-Mwanza KM 341, (kushoto), ni Mkurugenzi mkuu wa
TRC Bw, Masanja Kadogosa.
Muonekano wa mataruma ya zege yakiwa katika hatua za utengenezwaji
wake katika karakana ya Seke sehemu ya Isaka-Mwanza.
Eng. Christopher Kalist akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alipokagua ujenzi wa reli ya kisasa SGR
sehemu ya Isaka-Mwanza KM 341, (kushoto), ni Mkurugenzi mkuu wa
TRC Bw, Masanja Kadogosa.
Muonekano wa reli ya SGR na treni ya ufundi ambayo ujenzi wake
unaendelea sehemu ya Isaka-Mwanza.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akiteta jambo na
mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw, Adam Malima walipokagua jengo la abiria
katika kiwanja cha ndege cha Mwanza.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw, Adam Malima akimuonesha Waziri wa
Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa mandhari nzuri ya kiwanja cha
ndege cha Mwanza walipokagua jengo la abiria kiwanjani hapo.
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia
kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR sehemu ya
Isaka-Mwanza KM 341 na kuwataka wakazi wa kanda ya ziwa kujipanga
kutumia fursa hiyo ya uchumi.
Amesema wakati ujenzi wa SGR ukiendelea ni wakati wa wadau
mbalimbali kubuni fursa za kibiashara na kihuduma zitakazoendana na
matumizi ya treni mpya ya kisasa.
“Fursa za reli ni nyingi hivyo hakikisheni mnaziibua ili kuwezesha huduma
ya treni itakapoanza kufanyakazi kwa tija”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha amewataka wafanyakazi wa reli hiyo kuwa wazalendo kwa kuepuka
tabia za wizi kwani tabia hizo zinaweza kuchelewesha mradi na kuleta
hasara kwa Serikali na Mkandarasi.
Amesema ujenzi wa barabara za lami, meli katika ziwa Victoria, reli ya
kisasa (SGR) na uboreshaji wa uwanja wa ndege ni dhamira ya Serikali
kuunganisha mikoa na nchi jirani kwa usafiri wa njia zote hivyo ni vema
kwa watanzania kujivunia miradi hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw, Adam Malima amemshukuru Waziri
Mbarawa kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa miradi ya miundombinu
mkoani humo na kumuahidi kuboresha huduma za ulinzi na usalama
kwenye miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.
“Mheshimiwa Waziri sisi Mwanza tunajengewa daraja la Kigongo –Busisi,
meli za kutoa huduma ukanda wote wa ziwa Victoria, jengo la abiria katika
uwanja wa ndege na SGR ndio itapita juu hapa mjini hivyo tunafarijika sana
kwa kweli”, amesema Mkuu wa mkoa Malima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw, Masanja Kadogosa
amesema ujenzi wa sehemu ya tano ya SGR umefikia asilimia 23.4 na
kumhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wataendelea kumsimamia
mkandarasi kikamilifu ili kazi ikamilike kwa wakati na ubora unaokusudiwa.