Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini –TMA imetoa angalizo la vipindi vya upepo mkali unaofikia Kilomita 40 kwa saa na Mawimbi Makubwa yanayofikia Mita 2.0 katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Mamlaka hiyo imesema maeneo yanayotarajiwa kukumbwa na upepo huo ni pamoja na Mikoa ya Lindi,Mtwara,Tanga,Pwani na ikijumuisha visiwa vya Mafia.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA Rose Senyagwa amesema kuwa maeneo mengine ni Mkoa wa Dar es salaam na Visiwa vya Unguja na Pemba ambapo hali hiyo inatarajiwa kujitokeza kuanzia siku ya Kesho Ijumaa Jan 20 –Jan 23 mwaka huu.
‘Athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuathiri shughuli za uvuvi na usafirishaji katika maeneo ya bahari ya Hindi’amesema Senyagwa
Hata hivyo Mamlaka hiyo imetoa tahadhari kwa wananchi wanaofanya shughuli zao katika bahari ya hindi kuhakikisha wanachukua tahadhari katika kipindi hicho.