Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa David Silinde {Suti ya Bluu katikati} alipotembelea Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Kikundi cha ngoma kikicheza ngoma ya ya lizombe maarufu mkoani Ruvuma,ni utamaduni ambao unatakiwa kuridhishwa na kizazi cha sasa na kijacho
Kikundi cha ngoma kikitumbuiza ngoma ngoma halisi ya kabila la wangoni inayoitwa Ligihu ambayo ipo hatarini kutoweka kwa sababu wanaocheza ni wazee
Sanamu ya askari iliyojengwa ndani ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji,sanamu hii imejengwa kuwakumbuka askari wa JWTZ wapatao 56 waliofariki dunia eneo la Lumbule Songea wakati wanarudi katika vita ya Kagera mwaka 1979.
………………………………………..
Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kukuza utalii wa kiutamaduni
Utalii wa kiutamaduni hapa nchini bado haujapewa kipaumbele
ukilinganisha na nchi nyingine kama Afrika ya kusini ambayo utalii
huo umepiga hatua kubwa.
Mkoa wa Ruvuma una utajiri mkubwa wa utalii wa utamaduni
ukilinganisha utalii wa ikolojia,miongoni mwa vivutio vya utalii wa
utamaduni ni Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliopo katika eneo
la Mahenge Manispaa ya Songea.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe
anabainisha kuwa,wadau wa utalii katika Mkoa wa Ruvuma
wamekusudia kuanzisha na kukuza utalii wa kiutamaduni (cultural
tourism) sanjari na kuboresha maeneo yote ya kihistoria ili
kuendeleza utamaduni hatimaye maeneo hayo yaweze kuingiza
mapato baada ya watalii kutembelea kama ilivyo katika visiwa vya
Zanzibar.
Challe anasema,wadau wa utalii mkoani Ruvuma tayari
wameshatembelea maeneo muhimu ya kihistoria kama vile
Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Makumbusho ya Rashid
Kawawa,Maposeni,Luhira,Peramiho na Chandamali katika Wilaya ya
Songea ili kutambua maeneo ya kihistoria na umuhimu wake kwa
faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Huu ni mwanzo wa jukumu la kuziboresha kumbukumbu za kihistoria
katika mkoa wa Ruvuma na kuimarisha utalii wa ndani na nje lengo
likiwa ni kuutangaza mkoa wa Ruvuma’’,anasisitiza Challe.
Kwa upande wake Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya
Majimaji Bartazar Nyamusya anasema serikali imedhamiria
kuyafanya Makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa vita ya Majimaji
kuwa makumbusho ya mfano Tanzania kutokana na makumbusho
hayo kuhifadhi vifaa halisi na silaha halisi ambazo walitumia
mashujaa hao kupambana na wakoloni wa kijerumani.
“Hii ni Makumbusho pekee nchini iliyoanzishwa mwaka 1980 ambayo
imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika utamaduni
na historia ya mtanzania hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii
na nyingine zilizopo hapa nchini ”,anasisitiza Mhifadhi huyo.
Naye Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu
anabainisha zaidi kuwa Mji wa Songea ni miongoni mwa miji
michache nchini ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita ya Majimaji
na kwamba katika makumbusho hayo kuna ushahidi ambao
unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki
kikamilifu katika vita hivyo.
Anabainisha zaidi kuwa katika eneo la mashujaa wa majimaji
yamejengwa majengo mbalimbali ambayo yamehifadhiwa vifaa
ambavyo ni mila na utamaduni wetu vilitumiwa na mashujaa hao ili
kuwaletea watanzania uhuru.
Maligisu anasema ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kuna
mnara wa kumbukumbu ya wanajeshi ambao walitoka Songea
kwenda kupigana vita ya Idd Amini kati ya mwaka 1978 hadi 1979
ambapo wakati wanarudi baada ya kushinda vita hiyo walipata ajali
mbaya na kufariki dunia askari wote 56 katika milima ya Lukumbulu
wilayani Songea.
Amesema Ili kuwakumbuka mashujaa hao serikali ilijenga mnara
katika eneo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ambako walizikwa
mashujaa wa vita ya majimaji kama sehemu ya kuwakumbuka hivyo
kurithisha mila,ushujaa na utamaduni wa mtanzania.
Kulingana na sera ya utamaduni ya mwaka 1997 pamoja na sheria
ambayo inayatambua maeneo haya serikali imeamua mji wa Songea
uingizwe katika vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa ajili ya
kuendeleza historia ya Mji wa Songea ili uwe wa kihistoria, kishujaa
na kiutamaduni.
Utafiti uliofanywa na Makumbusho ya Taifa umebaini kuwa mji wa
Songea una vigezo vyote vya kuingizwa katika rasilimali za
kiutamaduni za taifa,ili kuhakikisha kuwa watalii wengi wa ndani na
nje ya nchi wanafika katika makumbusho hayo ili kujifunza utamaduni
wa mtanzania.
Hali ya mila,utamaduni na desturi iliyopo kwa vijana wa sasa katika
nchi yetu ni mbaya kwa kuwa vijana wengi wamesahau utamaduni
mila na desturi za mtanzania na kuendekeza mila za kigeni ambazo
zimeharibu kabisa maadili mema ya mtanzania.
Mbunge Jimbo la Nyasa Injinia Stella Manyanya anasema
uhamasishaji wa kufufua utalii wa kiutamaduni kusini unaendelea ili
kuhakikisha watu wa rika zote wanatembelea vivutio mbalimbali za
utalii ikiwemo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.
Injinia Manyanya ameipongeza Idara ya Makumbusho ya Taifa ya
Majimaji kwa kuandika barua kwa wakuu wa shule katika mkoa wa
Ruvuma ili kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kutembelea
vivutio vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali ili kupenda utalii
tangu wakiwa wadogo.