Afisa Elimu Maalumu Mkoa wa Dar es salaam,Swalehe Msechu (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe wakizindua mradi wa mazoezi Tiba katika kituo cha usonji cha Msimbazi Mseto kilichopo jijini Dar es salaam ulioratibiwa na Lukiza Autism Foundation.
Picha ya pamoja Afisa Elimu Maalumu Mkoa wa Dar es salaam,Swalehe Msechu (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe wakiangalia jambo wakati wa uzindua mradi wa mazoezi Tiba katika kituo cha usonji cha Msimbazi Mseto kilichopo jijini Dar es salaam ulioratibiwa na Lukiza Autism Foundation.
………………
NA MUSSA KHALID
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuandaa Mazingira wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalumu ikiwa ni pamoja na kuondokana na dhana potofu juu ya watoto hao katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Afisa Elimu Maalumu Mkoa wa Dar es salaam,Swalehe Msechu wakati akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa mazoezi Tiba katika kituo cha usonji cha Msimbazi Mseto ulioratibiwa na Lukiza Autism Foundation ambapo amesema kwa sasa Jamii imeendelea kuwa na uelewa kuhusu watoto wenye mahitaji hayo.
Msechu amesema tangu serikali ilipoanza mchakato wa ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu 2018 imesaidia kuongezeka kwa watoto wanaoandikishwa shuleni kwa ngazi ya awali.
‘Wazazi na wanajamii wote nitoe wito kwao kwamba waone jinsi watoto waliopo mashuleni wanapata huduma tofauti na waliopo nyumbani kwa hiyo wakishaona haya watavutika na kuwaleta watoto shuleni ili waweze kujipatia huduma ya elimu’amesema Msechu
Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu mwanzoni zilikuwa zipo chini lakini kwa sasa zinaendelea kuongezeka kuandikisha watoto wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe amesema katika kutambua Umuhimu wa Elimu jumuishi Taasisi hiyo imeandaa mradi wa mwaka mmoja ili kusaidia watoto wenye usonji.
‘lengo letu ni kuja kuzindua mradi wa mwaka mmoja wa mazoezi tiba katika kituo cha usonji msimbazi Mseto ambapo tutakuwa tunalipia mazoezi tiba ya mawasiliano na mazoezi tiba kazi kwani tunajua changamoto kwa watoto hawa tutawapa usafiri ili kuwarahisishia huduma’amesema Nkabe
Nkabe amesema Mill 100 waliyoipata kwa ajili ya kuwasaidia vijana wenye usonji wamechangishiwa na mwanafunzi wa Kidato cha nne katika Shule ya Kimataifa ya Internationa School of Tanganyika Madelin Kimario ambaye mradi wake uliendana na mradi wao.
‘Mwanafunzi huyo katika shule alikuwa akitaka kufanya mradi wa kuhusiana na usonji na kuisaidia jamii na alitusaidia sisi kutusaidia hizo fedha ili tuweze kukamilisha mradi wetu huu kwa pamoja’ameendelea kusema Nkabe
Katika hatua Nyingine Lukiza Autism Foundation imeandaa mbio za hisani zilizopewa jina la “Run for Autism Tanzania” zinazotarajiwa kufanyika April 30 mwaka huu.