Mwenyekiti wa TAMIDA ,Sammy Mollel akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
…………………………….
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Wadau wa madini ya Tanzanite wameiomba serikali kutumia taasisi zake kudhibiti watu wanaoeza taarifa za upotoshaji kwamba madini ya Tanzanite yanaendelea kutoroshwa kwa wingi licha kuwepo kwa udhibiti mkubwa katika uchimbaji na uuzaji wa rasilimali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa,Mwenyekiti wa Chama cha wanunuzi na wauzaji madini Tanzania(TAMIDA) ,Sammy Mollel amesema athari za kuendelea kufumbia macho upotoshaji huo ni kubwa na licha ya kuendelea kudumaza soko la madini hayo kitaifa na kimataifa zinazoofisha jitihada zinazoendelea za kukuza uchumi na pato la Taifa.
Mollel amesema kuwa ,wao kama wadau sekta hiyo wamesikitishwa na taarifa hizo na amewataka watanzania kutoa ushirikiano ukiwemo wa kuwabaini watu wanaoeneza taarifa hizo ama kusaidia kubaini ukweli wa utoroshaji huo ili hatua ziweze kuchukuliwa.
“Tangu kujengwa kwa ukuta katika eneo hilo mwaka 2017 na kufungwa kwa mitambo ya kielektroniki ya ulinzi kumesaidia sana kuondoa mianya ya utoroshaji wa madini na kwa hali inayoonekana hapa hakuna utoroshaji unaoweza kufanyika kutokana na udhibiti mkubwa uliopo, taasisi zote za serikali zipo,mifumo yote imekamilika na inafanya kazi, huo utoroshaji unaodaiwa unafanyika wapi na kwa njia gani? alihoji Mollel na kuongeza kuwa kuna haja ya kufuatilia na kuchukua hatua”amesema Mollel.
Ameongeza kuwa,kama mtu ana uhakika na taarifa hizo ni vizuri akatoa ushirikiano kwa kutoa ushahidi namna madini hayo yanatoroshwa pamoja na kuonyesha mianya yote inapopitia ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua na sio kutoa taarifa za kupotosha ambazo kwa tafsiri nyingine zinadhalilisha kazi yote iliyofanyika na uwekezaji wote uliopo na watendaji wote walioaminiwa wanaofanyakazi katika eneo hilo.
“Kuna udhibiti mkubwa sana unaofanyika kuanzia chini ya ardhi hadi kufikia sokoni huku zoezi hilo likisimamiwa na maafisa na watalaam kutoka taasisi zaidi ya saba kwa lengo la kuhakikisha hakuna utoroshaji wowote wa madini ya Tanzanite unaoweza kufanyika na sisi hatutaki kukanusha bali tunataka ukweli uulikane na kama utoroshaji upo udhibitiwe na kama haupo wapotoshaji wachukuliwe hatua .ili lengo liweze kutimia na watanzania wanufaike na Rasilimali hiyo .”alisiistiza Mollel.
Naye Afisa madini mkazi Mirerani ,Menard Msengi amesema kuwa,serikali imeweka ulinzi wa kutosha na mazingira mazuri kuanzia kwenye miradi hadi kufikia sokoni katika kuhakikisha sheria zote zinafuatwa na kwa ulinzi uliopo swala la utoroshaji haliwezi kufanyika hata kidogo .
Amesema kuwa, soko kubwa la madini ya Tanzanite hivi sasa lipo nchini Marekani ambapo kutokana na taarifa hizo za upotoshaji ambazo zinatolewa na watu wasio na nia njema na Watanzania zinalengo la kuharibu biashara hiyo ambayo ilikuwa unaenza kushika kasi katika masoko ya kimatafa likiwemo la marekani
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wanunuzi wadogo wadogo wa madini Tanzania(CHAMATA),Jeremia Kituyo amesema taarifa za kuwepo kwa utoroshaji wa madini zinasababisha washindwe kufanya biashara kwani zinawaondolea uaminifu kwa wateja wao na wamesisitiza umuhimu vyombo vinavyohusika kufuatilia na kudhibiti tatizo hilo
“Tunasikitika sana na matamko yanayotolewa yasiyo na ushahidi kwamba madini yanatoroshwa ,ambapo yanatufedhehesha na kutuvunja moyo na kuharibu sura ya biashara ya madini nchini,ambayo matamshi hayo wanaweza kusababisha mataifa mengine kuona kama madini yetu yana migogoro kitendo ambacho sio kweli”amesema Kituyo.
Mhandisi migodi kutoka kampuni ya Franone Mining,Benezet Karyuka amesema kuwa, tangu kuwepo kwa ukuta uliojengwa na serikali almaarufu kama ukuta wa Magufuli pamoja na kuondoa utoroshaji wa madini umewasaidia kuongeza ulinzi ndani ya maeneo ya uchimbaji.
Baada ya kuwepo kwa uchimbaji holela wa madini hayo ya tanzanite kwa muda mrefu serikali iliamua kufanya maboresho makubwa katika uchimbaji na uuzaji wa madini hayo yakiwemo ya kuweka ukuta na kumarisha mifumo ya uchimbaji ikiwemo kuweka utaratibu wa kuwatambua wachimbaji wakubwa na wadogo.
Pia katika maboresho hayo serikali imeweka utaratibu wa kuweka mnyororo wa kusimamia madini hayo kuanzia uchimbaji chini ya ardhi,usafishaji, uthaminishaji,na uuzaji, ambao umekuwa ukisimamiwa na wataalamu na watendaji wa taasisi zote zinazohusika, ulinzi wake pia unasimamiwa na taasisi zote za ulinzi na usalama wa Taifa .