Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la ubunifu katika mifumo ya
uendeshaji wa shughuli za kifedha duniani kote kutokana na maendeleo ya teknolojia.
Mojawapo ya ubunifu unaotawala katika mijadala ya kisasa ya kisera ni fedha ya
kidijitali ya benki kuu (Central Bank Digital Currency [CBDC]). Ijapokuwa inafafanuliwa kwa njia mbalimbali, CBDC ni aina ya fedha ya kidijitali katika nchi inayotolewa na kudhibitiwa na benki kuu. Kwa hiyo, inapotolewa, CBDC inakuwa fedha halali, sawa na fedha ya kawaida inayoshikika. Kulingana na maandiko mbalimbali ya kitaalamu, CBDC inaelezwa kuwa na faida nyingi kwa uchumi.
Kwa kuzingatia ukweli kwamba CBDC inaweza tu kutolewa na benki kuu, hivyo, kuwa chini ya mamlaka yake, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikitafiti uwezekano wa kutoa CBDC yake. Katika hatua hii ya utafiti, Benki Kuu ya Tanzania iliunda timu ya wataalamu wa fani mbalimbali kuchunguza vipengele vya kiutendaji vya CBDC na kuijengea uwezo timu hiyo kwa njia mbalimbali.
Pia, katika kuongeza uelewa wa CBDC kwa umma, Benki Kuu ya Tanzania iliandaa Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini Tanzania mwaka 2021 ukiwa na mada kuhusu CBDC na fedha za kidijitali (crypto). Aidha, Benki Kuu ya Tanzania ilikutana na wadau wa sekta ya fedha nchini ili kupata maoni yao kuhusu suala hili.
Pia, Benki Kuu imenufaika na mikutano mbalimbali ya kimataifa kama vile ya Kamati ya Magavana wa Benki Kuu ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Kamati ya Masuala ya Fedha ya Sekretarieti
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) kupitia Kituo cha IMF cha kanda (IMF AFRITAC), na Muungano wa Benki Kuu za Afrika. Benki Kuu ya Tanzania pia ilifanya vikao kadhaa na kampuni binafsi za kimataifa zinazotoa miundombinu na ufundi kwa CBDC.
Mambo muhimu yaliyozingatiwa wakati wa hatua hii ya utafiti ambayo Benki Kuu ya Tanzania inaendelea nayo ni kuchagua namna inayofaa katika kutumia CBDC kulingana na muktadha wa Tanzania. Hii inahusisha aina ya CBDC itakayotolewa (jumla, rejareja au mchanganyiko wa zote mbili), miundo ya utoaji na usimamizi (ya moja kwa moja, isiyo ya moja kwa moja, au ya mseto), aina ya CBDC (token-based au account based), muundo (remunerated au non-remunerated) na kiwango cha uwazi au ufuatiliaji.
Aina itakayochaguliwa inapaswa kuzingatia vihatarishi vya utoaji wa fedha ya
kidijitali ya benki kuu na njia za kudhibiti hivyo vitahatarishi katika utoaji na utumiaji wa fedha hiyo.
Matokeo ya utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania yalibainisha kuwa zaidi ya nchi 100 duniani ziko katika hatua tofauti za kutaka kutumia fedha ya kidijitali ya benki kuu, 88 zikiwa katika utafiti, 20 katika uthibitisho wa dhana, 13 katika majaribio na 3 katika Uchambuzi wa matokeo haya unaonyesha kuwa benki kuu nyingi duniani zinakwenda kwa tahadhari katika utekelezaji wa mpango wao wa kutaka kutumia fedha ya kidijitali ya benki kuu (CBDC) ili kuepuka hatari zozote zinazoweza kuvuruga utulivu
na usalama wa uchumi wao.
Pia, ilionekana kuwa, nchi 6 zilighairi kutumia CBDC hasa kutokana na changamoto za kimuundo na teknolojia katika awamu ya utekelezaji. Changamoto za kimuundo ni pamoja na kutumia fedha taslimu katika kufanya miamala, kuwepo kwa mifumo isiyofaa ya malipo, gharama kubwa ya utekelezaji na viashiria vya hatari vya mfumo wa utoaji wa fedha uliopo.
Katika kuzingatia hili, Benki Kuu ya Tanzania imeamua kutumia mbinu ya kwenda hatua kwa hatua, ikichukua tahadhari na kuzingatia vihatarishi katika kutumia fedha ya kidijitali ya benki kuu. Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kufuatilia, kutafiti na kushirikiana na wadau, zikiwemo benki kuu nyingine, katika jitihada za kufikia matumizi ya fedha ya kidijitali ya benki kuu na kuchagua teknolojia stahiki kwa ajili ya utoaji wa shilingi ya Tanzania katika mfumo wa kidijitali.
Baada ya kuhitimisha awamu ya utafiti, Benki Kuu ya Tanzania itatoa taarifa kwa umma kwa ujumla juu ya namna ya kusonga mbele.
Taarifa hiyo inaweza kujumuisha mpangokazi katika kuanzisha fedha ya kidijitali
ya benki kuu (CBDC) nchini.