Mwakilishi wa Mradi wa BOOST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Gema Toddy akiwa katika kikao kazi cha wadau wa elimu waliokutana mjini Morogoro Januari 10 – 13, 2023 kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba akisalimiana na Mwakilishi wa Mradi wa BOOST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Gema Toddy mjini Morogoro katika kikao kazi cha kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu.
Mwakilishi wa Mradi wa BOOST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Gema Toddy (kushoto) akiwa na Mratibu wa Mradi huo kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Neema Lemunge wakati wa kikao kazi cha kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kilichofanyika Januari 10 – 13, 2023 mjini Morogoro.
Washiriki wa Kikao Kazi cha kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kilichofanyika mjini Morogoro Januari 10 -13, 2023 wakiwa katika vikundi kwa ajili ya kupitia rasimu ya ufafanuzi huo na kuiboresha.
Washiriki wa Kikao Kazi cha kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kilichofanyika mjini Morogoro Januari 10 -13, 2023 wakiwa katika vikundi kwa ajili ya kupitia rasimu ya ufafanuzi huo na kuiboresha.
Mwenyekiti wa Kikao wa Kikao Kazi cha kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kilichofanyika mjini Morogoro Januari 10 -13, 2023, Wakili Richard Odongo akizungumza na washiriki (hawapo pichani) wa kikao kazi hicho juu ya namna ya kupitia rasimu ya ufafanuzi huo kipengele kwa kipengele.
Mmoja wa washiriki wa Kikao Kazi cha kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kilichofanyika mjini Morogoro Januari 10 -13, 2023, akichangia hoja kwa ajili ya kuboresha rasimu ya Ufafanuzi huo.
Na Mwandishi Wetu – Morogoro.
Benki ya Dunia ambayo ni mfadhili wa Mradi wa BOOST imeonesha kuridhishwa na namna Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) inavyotekeleza moja ya malengo ya mradi huo katika kuwasaidia walimu kuwa na mwenendo mwema unaozingatia miiko na maadili ya kazi hiyo.
Hayo yameelezwa na Mtaalamu wa Elimu kutoka Benki ya Dunia ambaye pia ni Msaidizi Mkuu wa Mradi wa BOOST, Gemma Todd wakati wa Kikao kazi kilichoandaliwa na TSC kwa lengo la kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu kilichofanyika Januari 10 – 13, 2023 mjini Morogoro.
Amesema kuwa Mradi wa BOOST unalenga kuimarisha na kuboresha elimu ya Awali na Msingi kwa shule za Serikali ambapo shughuli mbalimbali zimepangwa kuanyika ili kufikia lengo hilo, shughuli hizo ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, kuhakikisha shule zina usalama wa kutosha, kujenga shule mpya na madarasa mapya na kuhakikisha walimu wanapata mafunzo mara kwa mara na kwa karibu.
“Nimeshiriki kwenye warsha nzuri sana ambayo imeandaliwa na TSC kujadili maadili ya walimu wetu, tunajua watoto watashidwa kusoma wasipokuwa na usalama shuleni, pia wasipokuwa na walimu ambao wanaweza kuwa karibu nao na kuweza kuwaongoza vizuri. Kwa kweli warsha hii imekwenda vizuri na matokeo ya warsha hii ni kutusaidia kufikia malengo ya afua namba mbili ya mradi wetu ambayo inazungumzia shule salama”, alisema Todd.
Ameeleza kuwa katika mazingira ya sasa ambapo kumekuwa na mabadiliko ya kitabia yanayosababisha kuharibika kwa maadili katika jamii ni muhimu kuweka mkazo katika kusaidia walimu kuzingatia Miiko na Maadili ya kazi yao ili kufanya shuleni kuwa mahali salama kwa wanafunzi, hivyo TSC imefanya jambo la msingi sana kwa kuamua kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Maadili na Utendaji kazi wa Walimu.
“Kanuni za Maadili hayo zikifafanuliwa vizuri na kueleweka zitamwongoza mwalimu kutambua wajibu wake awapo shuleni au eneo lake la kazi kwa kuwa wajibu wake ni zaidi ya kufundisha darasani. Mwalimu anawajibika katika malezi ya mtoto kimwili, kiakili, kiroho, kijamii na kisaikolojia. Lakini pia ana wajibu kwa viogozi wake na wasimamizi wake wa kazi, anawajibika kwa jamii anamoishi na anawajibika kwa Umma au Taifa kwa ujumla. Haya yote yamejadiliwa kwa kina katika warsha hii,” alisema Todd.
Todd amefafanua kuwa pamoja na wajibu, walimu kama watumishi wengine wana haki zao ambazo ni lazima zilindwe na kutetewa ili watekeleze majukumu yao katika mazingira ya amani, furaha na utulivu, hivyo ni wajibu wa TSC pamoja na mamlaka zingine zinazosimamia walimu kuwaelimisha juu ya haki hizo ili waweze kuwajibika vizuri.
Mradi wa BOOST unafuata utaratibu wa lipa kutokana na matokeo, ikimaanisha kuwa kila mwaka Benki ya Dunia itukakaa na Serikali kupitia Wizara na Taasisi zinazotekeleza mradi huo kwa ajili ya kupima matokeo ya kazi zilizofanyika, hivyo fedha za mwaka unaofuata zitatolewa endapo matokeo ya upimaji huo yataonesha malengo yanatekelezwa vizuri.
“Tuna imani kubwa kwa namna TSC inavyotekeleza sehemu ya mradi huu na ni matumaini yetu kuwa matokeo ya hiki kinachofanyika nikuona walimu wakifanya kazi zao kitaaluma na kitaalam ili wanafunzi wapate ujuzi katika masomo yao lakini wawe mfano wa kuigwa kwa kuwa na maadili mema kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” alisema Todd.
Alimema kuwa mradi wa BOOST unatekelezwa na Wizara mbili ambazo ni Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) na kueleza kuwa Taasisi zilizo chini ya Wizara hizo zinazotekeleza mradi huo ni TSC, Taasisi ya Elimu Tanzania, Baraza la Mitihani Tanzania pamoja na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM).
Naye Mkurugezi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Bi. Fatma Muya amesema kuwa TSC iliandaa andiko la Mradi ambalo lilikubalika na kupata ufadhili ambapo alieleza kuwa moja ya kazi zilizokubalika kutekelezwa katika mradi huo ni kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu ambazo walimu wanapaswa kuzitekeleza ili kuboresha elimu na kuwa na shule salama.
“Kwa sasa tupo katika hatua ya kuandaa ufafanuzi huo na kwenye kikao kazi hiki tumewaita wadau mbalimbali waliobobea katika masuala ya elimu na Walimu wakiwemo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Elimu, Haki Elimu, Taasisi ya Elimu, ADEM, Taasisi ya Elimu Tanzania, Chuo Kikuu Dodoma, Chama cha Walimu Tanzania pamoja na wadau wengine waliobobea katika utumishi wa Walimu,” alisema Muya.
Amefafanua kuwa kazi inayofanyika katika kikao kazi hicho ni kupitia na kuboresha rasimu ya Mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu ambayo iliandaliwa na Menejimenti ya Tume hiyo na baada ya kikao kazi hicho, hatua itakayofuata ni kuchapisha na kusambaza vitabu shuleni pamoja na kutoa elimu kwa wadau mbalimbali.
Ameongeza kuwa TSC inatarajia kwamba ufafanuzi huo utasomwa na kueleweka kwa walimu wote kwa kuwa umeandikwa katika lugha rahisi na kutoa elimu kwa wadau juu ya Kanuni hizo, hivyo kila mwalimu ataelewa misingi ya kile anachopaswa kufanya katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa TSC, Bi. Neema Lemunge amesema kuwa pamoja na kazi ya kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili katika Utumishi wa Walimu, Mradi wa BOOST umefadhili utekelezaji wa shughuli zingine ikiwemo kufanya mapitia ya Sheria mbalimbali zinazohusu walimu, ununuzi wa vitendeakazi vikiwemo magari na kompyuta.