Naibu Kamishna wa TFS Emmanuel Wilfred amesema kuwa katika taasisi ushirikiano uliopo ndio msingi mkubwa ambao hupelekea malengo ya Taasisi kufikiwa kwa wakati kwani shughuli zote hufanyika kwa umoja.
Emmanuel Wilfred ameyasema hayo wakati alipotembelea Shamba la Miti SaoHill kwa ziara ya kikazi ili kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika shambani hapo.
Ameendelea kusema kuwa iwapo kuna changamoto zinajitokeza ni vyema kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa kwa pamoja na kwa wakati ili kufikia malengo ya taasisi kwa wakati na hivyo kufanya taasisi yenye umoja wakati wote.
“Mhifadhi uhakikishe mnafanya vikao kama hivi mara kwa mara kwani itasaidia kujua changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja na kwa haraka ili kuleta wahifadhi wote pamoja ambapo itasaidia kuleta utendaji kazi ulio na tija.” Amesema Naibu Kamishna Emmanuel Wilfred
Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa wahifadhi wote katika taasisi kuhakikisha wanafuata taratibu na miongozo iliyopo ili kusimamia utendaji kazi ambapo itasaidia kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza ambazo zitatokana na ukiukwaji wa taratibu zilizopo.
Amesisitiza kuwa taasisi inafanya biashara pia ya mazao ya misitu kupitia Shamba la Miti SaoHill hivyo wahifadhi wote wahakikishe wanawahudumia wateja wote vizuri na kwa wakati na kuhakikisha endapo kuna changamoto zozote zitakazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati ili kufikia malengo ya taasisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mhasibu Mkuu Fedha Peter Mwakyosa amesema kuwa wahifadhi wanatakiwa kuhakikisha wanatumia taaluma zao vizuri katika utendaji wao wa kazi wa kila siku ili kuhakikisha taribu zote zilizopo zinasimamiwa ipasavyo ili kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zinafanya malengo ya taasisi kutofikiwa kwa wakati.
Amesema kuwa kila Mhifadhi kuhakikisha anaendelea kuwa mbunifu na kununua namna mbalimbali katika kusimamia utendaji wa kazi ambao itapelekea utendaji kazi mzuri na wenye tija wakati wote kwa taasisi na taifa kwa ujumla.
“Kila mmoja akumbuke kuwa ameaminiwa na serikali katika jukumu tulilopewa la usimamizi wa rasilimali za misitu hivyo ni vyema tukaonesha uzalendo kwa vitendo katika kusimamia jukumu tulilopewa.”Amesema Kamishna Msaidizi Mwandamizi Peter Mwakyosa
Akishukuru baada ya kikao hicho Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti SaoHill Tebby Yoram amesema kuwa anaahidi kuendelea kusimamia sheria , taratibu na kanuni zilizopo na kuhakikisha changamoto ambazo zinajitokeza kutafutiwa ufumbuzi wa pamoja na kwa haraka ili kuendelea kuboresha mahusinao baina ya watumishi na wateja ili kufikia malengo ya taasisi.