Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akimwaga mchanga katika kaburi la aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa. Hafla ya maziko imefanyika leo tarehe 07 Januari, 2023 katika Kijiji cha Msemembo kilichopo katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
………………………………
Mary Gwera, Mahakama-Msemembo, Manyoni
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 07 Januari, 2023 ameongoza maelfu ya watu kumzika aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa aliyefariki dunia tarehe 02 Januari, mwaka huu.
Akizungumza na hadhara iliyokuwepo katika ibada ya kumuaga marehemu Jaji Utamwa katika kijini cha Msemembo Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Mhe. Siyani amesema kuwa, Mahakama imepoteza mtu makini ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwa Mhimili huo na Taifa kwa ujumla.
“Kwanza napenda kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwani tumepata pigo zito na tumempoteza Kiongozi, mwalimu na rafiki wa wengi ambaye alikuwa akipenda ushirikiano na watu katika masuala mbalimbali,” amesema Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi ameainisha kuwa, marehemu Jaji Utamwa alikuwa na mchango mkubwa kwa Mahakama na jamii, huku akieleza kuwa marehemu alipenda kufanya tafiti za masuala mbalimbali, alikuwa mwanahaki aliyependa kusimamia haki za watu bila kuwa na chembe ya ubaguzi.
“Marehemu Jaji Utamwa alipenda sana elimu kujiendeleza, licha ya kukaribia kustaafu mwaka jana alianza kusoma shahada nyingine, hili ni funzo kwetu kuwa elimu haina umri, mara nyingi alinishauri mimi pia nijiendeleze zaidi nami nilisikiliza ushauri wake na nimeanza shule na hivi karibuni alinitumia boksi la vitabu ili kunisaidia katika masomo yangu,” ameeleza Jaji Kiongozi.
Kiongozi huyo wa Mahakama Kuu ametoa ujumbe kwa Wana-Manyoni kuwa marehemu alikuwa Mtetezi wao, kwakuwa alipenda ustawi wa Wilaya yake huku akitoa mfano kuwa, marehemu Jaji Utamwa ndiye aliyejenga hoja zenye mashiko zilizosababisha kujengwa kwa Mahakama mpya ya Wilaya ya Manyoni ambayo Mhe. Siyani anabainisha kuwa marehemu Jaji Utamwa alitamani awepo wakati wa uzinduzi wa jengo hilo la Mahakama. Ameongeza kwa kuwasihi wananchi wa Wilaya hiyo kuyaenzi mazuri yote aliyokuwa nayo ikiwa ni pamoja na kutunza amani na haki aliyoidumisha.
Kwa upande wa familia, Mhe. Siyani amewasihi kuwa na moyo wa ushujaa huku akitoa neno la Faraja kwa familia hiyo kutoka Kumbukumbu la Torati sura ya 31 mstari wa sita (6) lisemalo; ‘Iweni Hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msihofu kwa maana Bwana Mungu wako yeye ndie anayekwenda pamoja nawe hatakupungukia wala kukuacha’.
Akiongoza misa ya mazishi ya Jaji Utamwa, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Bonde la Ufa (Lift Valley), Baba Askofu John Lupaa ameainisha mambo manne ya kumkumbuka marehemu ambayo ni pamoja na kuwa na heshima kwa watumishi wenzake wa umma ambapo aliamini kuwa kila mtu ana nafasi muhimu nkatika kazi, mchapakazi ambapo alitekeleza wajibu wake kwa weledi na uadilifu mkubwa, kuimarisha uhusiano kati ya Viongozi wa dini na Serikali na jambo la nne marehemu alikuwa Mkristo halisi aliyeshiriki katika mambo mbalimbali ya kikanisa.
Akisoma wasifu wa Marehemu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kwamba, marehemu alihudumu katika vituo mbalimbali vya kazi huku akishika vyeo mbalimbali ikiwemo uhakimu, usajili na kadhalika na hadi umauti unamfika alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.
Kadhalika, Prof. Ole Gabriel ametoa shukrani kwa ndugu, jamaa marafiki, Madaktari, kanisa, watumishi wa Mahakama na wananchi kwa ujumla kushiriki kwa karibu katika kipindi chote cha kumuuguza marehemu Jaji Utamwa hadi kuzikwa kwake.
Baadhi ya Viongozi wengine waliotoa salaam za rambirambi ni pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba, Mwakilishi wa TLS na kadhalika ambao kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa marehemu atakumbukwa kwa mchango wake katika tasnia ya sheria nchini ambapo alisimamia haki kwa dhati na hata hukumu alizotoa zilikuwa kama mwongozo kwa wanasheria.
Marehemu amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la Damu ambapo tarehe 17 Desemba, 2022 alilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Mnamo tarehe 18 Desemba, 2022 alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kuendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomfika.
Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alizaliwa tarehe 30 Juni, 1963 na alijiunga na Mahakama ya Tanzania tarehe 17 Februari, 1992
Akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alifanya kazi katika kanda za Dar es Salaam, Tabora, Mbeya na Iringa. Marehemu ameacha mjane na Watoto watano (5) na mjukuu mmoja (1).
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakisaidiana kubeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa aliyefariki dunia tarehe 02 Januari, 2023. Ibada ya maziko imefanyika nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Msemembo Manyoni mkoani Singida.
Viongozi wa dini wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Bonde la Ufa (Lift Valley), Baba Askofu John Lupaa (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika ibada ya maziko ya marehemu Jaji Utamwa.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza wakati wa ibada ya maziko ya marehemu Jaji Utamwa.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda akizungumza jambo katika tuki hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego akitoa neno katika ibada hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiaga mwili wa Jaji Dkt. Utamwa kabla ya maziko.