Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (MB) akiongea pamoja na kujibu maswali katika mikutano ya hadhara na wananchi wa Kata ya Baleni, Kijiji cha Kungwi na Kata ya Mibulani wilayani Mafia wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa TBC na uhakiki wa Anwani za Makazi juzi Januari 5, 2023
………………………..
Na Immaculate Makilika – MALEZO, Mafia
Wilaya ya Mafia iliyopo mkoani Pwani inatajwa kunufaika na ujenzi wa minara ya mawasiliano itakayojengwa katika wilaya hiyo ili kutatua changamoto ya mawasiliano.
Akizungumza juzi (Januari 5, 2023) katika Shule ya Sekondari Kilindoni iliyopo katika Kata ya Kilindoni wilayani Mafia wakati akiwa kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya mawasiliano, ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, usikivu wa redio TBC na uhakiki wa anwani za makazi.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi katika ujenzi wa minara ya mawasiliano ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Akitolea mfano mnara wa mawasiliano wa Kampuni ya Simu za Mkononi wa Halotel uliopo katika shule hiyo ya Sekondari ya Kilindoni ambao umejengwa na Kampuni ya Halotel kupitia ruzuku iliyotolewa na UCSAF amesema “Serikali kupitia UCSAF iliingia makubaliano na Halotel kujenga mnara huu unaotarajiwa kukakamilika mwishoni mwa mwezi wa Januari, 2023. Aidha, mnara mwingine utakaowashwa pamoja na huu upo katika Kijiji cha Banja kata ya Kirongwe na kwa pamoja utawezesha wananchi wa vijiji hivi na jirani kuanza kupata huduma hadi za 3G”.
Naye, Mratibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kanda ya Pwani, Mhandisi Mwandamizi Baraka Elieza amesema kuwa lengo la UCSAF ni kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo kampuni za simu za mkononi hazikuwa zinapeleka huduma kutokana na sababu za kibiashara.
“Tayari UCSAF imeingia mikataba mbalimbali na makampuni ya simu kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 1,235 nchi nzima na tayari minara katika kata 1,031 imewaka, huku katika Wilaya ya Mafia ikiwa minara mitatu kati ya hiyo. Aidha Serikali kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali ulizijumuisha kata za Jibondo, Miburani, Kirongwe na Baleni katika zabuni ya miradi iliyotangazwa mwezi Oktoba mwaka 2022 na zabuni hiyo inatarajiwa kufunguliwa Januari 31, 2023 na mara itakapokamilika itataua changamoto ya mawasiliano katika kata hizi”. Ameeleza Mhandisi Baraka.
Kwa upande wake, Mkazi wa Dongo, Kitongoji cha Ngemeni, Bw. Maulid Seleman ameeleza kuwa mnara huo uliopo Kata ya Kilindoni utakapoanza kutoa huduma itasaidia wakazi wa eneo hilo na kutoa fursa mbalimbali zinazotokana na mawasiliano.
Aidha, Naibu Waziri Mheshimiwa Mhandisi Kundo Mathew amemaliza ziara yake ya siku moja wilayani Mafia ambapo anaendelea na ziara hiyo leo Januari 7, 2023 katika Mkoa wa Morogoro.