……………………..
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameipongeza sekta binafsi kwa jitihada mbalimbali inazozichukua kuhifadhi misitu hapa nchini akieleza kuwa Serikali inayoongozwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini jitihada hizo.
Mhe. Balozi Dkt. Chana ameyasema hayo wakati kikao chake na Wadau wa Misitu kutoka Sekta binafsi kilichofanyika jijini Arusha.
Ameeleza kuwa wadau wa Misitu kutoka Sekta Binafsi wanachangia katika uhifadhi wa mazingira, kukuza uchumi wa nchi na kipato cha mtu mmoja mmoja akiongeza kuwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua akiwaunga mkono kwa vitendo kwa kuhamasisha uhifadhi na maendeleo ya rasilimali za misitu hapa nchini.
Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta 48.1 milioni za misitu ambayo imekua muhimili wa shughuli nyingi za kiuchumi zinazogusa moja kwa moja maisha ya watu kama upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali na kutoa rai wa jamii Kutumia bidhaa zinazotokana na Misitu nchini kwa kuwa ni nzuri na imara.
“Maliasili za misitu zimekuwa na manufaa kwa kila Mtanzania pia zimekua zikichangia kwa kiasi kikubwa kwenye Pato la Taifa, hata hivyo juhudi za kuendeleza misitu ya asili pamoja na ya kupandwa zimekuwa zikikumbwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi”. Alisema Waziri Balozi Dkt. Chana.
Mhe. Balozi Dkt. Chana amesema ni imani yake kuwa Wadau wa Sekta Binafsi wataendelea kutumia taaluma na rasilimali zao kwa weledi katika kusimamia uhifadhi na kuanzisha na kuendeleza viwanda vya mazao ya misitu ili kufikia malengo ya idadi ya viwanda 252 ifikapo mwaka 2031 kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa EWPs.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Sekta binafsi Bw. Ben Sulus ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kukutana na Wadau kutoka sekta binafsi Ili kubadilisha uzoefu hivyo anaamini kikao hicho kitaleta matokeo chanya katika kuinua sekta ya Misitu ili izidi kuchangia katika pato la Taifa.