Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kushoto) akizungumza na uongozi wa juu wa Kampuni la usambazaji wa mbolea la ETG akiwa katika ghala wanalolitumia kuhifadhi na kuuza mbolea ili waweze kufikisha mbolea hizo katika maeneo ya pembezoni wakishirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa jambolililoanza utekelezaji wake mapema baada ya Waziri Bashe kuondoka katika eneo hilo na kuweza kufikisha mbolea Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Aliyeshika simu ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kulia) akisikiliza taarifa ya usambazaji wa mbolea katika Mkoa wa rukwa kutoka kwa Afisa Masoko wa kampuni la OCP mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Zawadi Hankungwe
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza jambo ofisini kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (kulia) mara baada ya kuangalia taarifa za upatikanaji wa mbolea katika mkoa wa Rukwa kupitia mfumo wa usambazaji wa mbolea za ruzuku. Mwenye sweta la mistari ni Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Michael Sanga
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kushoto) akimsikiliza Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Michael Sanga akifafanua jambo wakati wa kikao kifupi na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (hayupo pichani).
………………………..
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amefanya ziara mkoani Rukwa na kutatua changamoto za wakulima kufuata mbolea maeneo ya mjini pamoja na uwepo wa watendaji wachache kwenye vituo vya mauzo ili kuwawezesha wakulima kuhudumiwa kwa wakati.
Katika ziara hiyo ya siku mbili, Waziri Bashe alitembelea maghala ya mbolea ya kampuni za ETG na OCP na shamba la mbegu la mwekezaji mkubwa la Msipazi Farm lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani humo.
Baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga kueleza nia ya kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa usafiri na kuwahakikishia ulinzi wafanyabiashara ili waweze kupakia na kupeleka mbolea maeneo ya pembezoni na wafanyabiashara kutokukubaliana na wazo hilo, Waziri Bashe aliagiza jambo hilo lifanyike na utekelezaji wake umeanza mapema baada ya maelekezo yake.
Kwa upande wa changamoto ya kupata mbolea ya ruzuku kwa wazalishaji wa mbegu katika scheme ya Msipazi Farm Waziri Bashe alimtaka mwekezaji Yusuph Sumrry kuandika barua ya mahitaji yake ya mbolea kwa Mkurugenzi wa TFRA ili kuyaridhia na kumwezesha kupata mbolea ya ruzuku.
“Andika barua kwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhusiana na ombi la kupata mbolea ya ruzuku atakuidhinishia ili wasambazaji wakuletee kiasi cha mbolea mnachokihitaji” Alisisitiza waziri Bashe.
Akikazia katika jambo hilo Waziri bashe alisema nchini kuna changamoto ya mbegu hivyo mwekezaji huyo atasaidia katika kuhakikisha wakulima wanapata mbegu kwa bei himilivu na kwa wakati kuliko kutegemea kuagiza kutoka nje ya nchi.