Na Mwandishi wetu, Mirerani
MCHIMBAJI wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Mkoani Manyara, Charles Mullo (Kichunga) amemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera, msaada wa vifaa 100 vya wanawake vya kujifungua ambao hawana uwezo.
Vifaa hivyo vya thamani ya sh2.8 milioni vitatumiwa na wanawake 100 wajawazito wasiojiweza kifedha vimetolewa na mchimbaji huyo Mullo kwa ajili ya kutumika kwenye kituo cha afya Mirerani.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Serera ambaye naye amemkabidhi mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya Mirerani, Dkt Deogratius Mazengo kwa ajili ya matumizi hayo.
Mullo amesema anatambua kituo hicho kinauhitaji hivyo wadau wa madini wanapaswa kusaidia hivyo wanachangia ili kuwasaidia wanawake hao 100.
Amesema vifaa hivyo vitawasaidia wanawake 100 ambao hawana uwezo wa kujinunulia vifaa hivi kwani mama mjamzito anapaswa kuwa na vifaa hivyo pindi akijifungua.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt Serera amemshukuru Mullo kwa kutoa vifaa hivyo kwani vitawasaidia wanawake hao watakaozalishwa katika kituo hicho cha afya Mirerani.
Amesema gharama ya vifaa hivyo ameambiwa ni sh2.8 milioni ila thamani yake ni kubwa mno kwani itawasaidia wanawake 100 kujifungua na kupata watoto kupitia msaada huo.
“Kwa kweli alichofanya mchimbaji huyu ni kusaidia jamii na serikali ambayo inapambana kuhakikisha inaondokana na tatizo la vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua hongera sana,” amesema Dkt Serera.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani Rachel Njau amempongeza mchimbaji hyo Mullo kwa kutoa vifaa hivyo
Njau amesema mchimbaji huyo ametumia kiasi cha fedha alichokipata kupitia madini ya Tanzanite, kurudisha kwa jamii (CSR) hivyo kudhihirisha wachimbaji wanavyojitoa kwa jamii.