Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewahikikishia wadau wa sekta ya habari kuwa kutakuwa na marekebisho ya sheria ya huduma za habari yanakwenda kufanyika Januari 2023 katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Nnauye alisema kuwa ili kuboresha sekta ya habari serikali imepanga kufanya marekebisho ya sera ili kuendana na wakati uliopo.
Alisema kuwa mabadiliko ya sheria ya habari ni mwanzo wa utatuzi wa changamoto za wadau wa habari na wanahabari wenyewe.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Samson Kamalamo alisema mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari itakuwa mwanzo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo katika sekta ya habari.
Kamalamo alisema kuwa mabadiliko yatakayofanyika Januari 2023 hayatakuwa ya mwisho, bali kadri muda unavyokwenda, yatahitajika mabadiliko mengine ambayo yataifanya sheria hiyo kwenda na wakati husika.
Alisema kuwa mabadiliko hayo hayatakuwa mwarobaini, isipokuwa itakuwa mwanzo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo katika sekta ya habari na kuiboresha na itakuwa mwanzo kujifunza kwa watu waliofanikiwa katika sekta ya habari.
“Tukijua wenzetu wamefanikiwa vipi, tunaweza tuka-copy, tukayaleta yale mazuri kwetu na kuiboresha. Kwa hiyo, haitakuwa mwisho wa kuiboresha, kwa hiyo watakwenda kupitisha sheria na hayo mabadiliko lakini bado mabadiliko mengine yatahitajika huko mbele kulingana na wakati,” amesema.
Kamalamo ameongeza kwamba mambo mengine katika sheria hiyo ni mazuri na angependa kuona yakiendelea, hususan kuitambua tasnia ya habari kama taaluma, jambo ambalo amesema linahitaji kulindwa
“Tumeanza kuona mwanga kwamba hata kule ambako tunafanya kazi bila kuajiriwa wanaweza kuona kumbe watu wa sekta hii wanapaswa watambuliwe kwamba uandishi wa habari ni taaluma kama nyingine,” amesema.
Naye Mhariri Msaidizi wa Habari wa gazeti la The Citizen, Louis Kolumbia amesema ana imani na serikali kwamba inakwenda kufanyia kazi mapendekezo ya wadau kwa sababu ameuona utashi wa kisiasa wa Rais Samia Suluhu Hassan.