MWENYEKITI wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa Frank Leonard amesema hatua ya serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kukubali kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni kandamizi zinazozuia vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru kumeanza kuwarudishia pumzi inayowafanya waandishi waweze kutimiza wajibu wao kama mhimili wa nne wa dola.
“Nikiri kwamba yapo mambo mengi katika sheria hizo ikiwemo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 yanahitaji maboresho,” alisema Leonard ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Alisema marekebisho ya sheria na kanuni hizo ambayo sehemu yake yanatarajiwa kuwasilishwa katika kikao kijacho cha bunge ni ya msingi ambayo yanapaswa kutizamwa kwa mawanda mapana.
kitoa mfano wa baadhi ya vifungu vinavyolalamikiwa Leonard alisema katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo, pamoja na mambo mengine, inaruhusu Serikali kufungia magazeti.
Sheria hiyo pia inaweka sharti kwa gazeti kuwa na leseni ambayo inapaswa ihuishwe kila mwaka. Pia, inaweka sharti kwamba ili mtu afanye uandishi wa habari Tanzania ni lazima awe na elimu ya kiwango cha stashahada au shahada ya uandishi wa habari au taaluma inazohusiana nazo.
Kingine kinacholalamikiwa ni Kanuni za Mawasiliano na Kielektroniki na Posta, Maudhui ya Mtandaoni za 2020 ambazo pamoja na kuipa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kufungia redio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kukiuka vitu kama vile “maadili ya taifa” pia zinaweka sharti kwa vyombo vya mtandaoni kuwa na leseni inayohuishwa kila mwaka ambayo gharama yake imekuwa ikilalamikiwa na wadau.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kupokea malalamiko ya wadau kuhusu sheria hizo na kuagiza zianze kufanyiwa marekebisho ili kuweka mazingira safi kwa wanahabari kufanya kazi zao,” alisema.
Katika kongamano la habari lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliahidi sheria hizo kuanza kufanyiwa maboresho katika kikao kijacho cha bunge Mwaka ujao 2023.H
Hatua ihiyo mekuja baada ya wadau wa habari Tanzania kuwasilisha serikalini mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko ya sheria ya habari kwa lengo la kuondosha vifungu kandamizi dhidi ya watoa huduma wa sekta hiyo.