Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi ametembelea wagonjwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road ili kuwajulia hali na kutoa misaada ya sikukuu kwa niaba ya familia yake.
Akizungumza mapema leo alipotembelea wagonjwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Prof. Makubi amesema kuwa ili kutilia mkazo jitihada hizo, serikali tayari imekwishaanza ujenzi wa vituo vingine katika katika Hospitali Kanda ya Rufaa Mbeya,KCMC Kilimanjaro, Bugando Mwanza na Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma.
Prof. Makubi amewapa zawadi mbalimbali pamoja na kunywa nao Chai kama kielelezo cha kuwatia moyo na kuwatakia ahueni kwenye matatizo yanayowasumbua na kufanya ibada fupi ya kuwaombea baraka ya uponyaji toka kwa mwenyezi mungu. Aidha aliwafahamisha ya kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan anafahamu changamoto za wagonjwa wa Saratani nchini hivyo anaendelea kusimamia maboresho katika Sekta ya Afya katika kutoa elimu kwa jamii, kubaini mapema, kutibu na kuimarisha Tiba Shufaa Kwa wagonjwa wa Saratani nchini Tanzania. Katibu Mkuu pia alitoa salamu za pole kwa wagonjwa toka kwa Waziri wa Afya, mheshimiwa Ummy Mwalimu.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa waliopo kwenye wodi wamemshukuru Prof.Makubi aliyeambatana na Familia yake na pia Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Prof Paschal Ruggajo kwa kuungana nao kwenye chai na kuwa kitendo cha kuwajali na wamefarijika sana leo kwa ziara yake hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Julius Mwaiselage alielezea maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika Taasisi hiyo kwa kusimamiwa na Serikali ya Awamu ya 6 inayosimamiwa na Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan ikiwemo kujenga majengo na kufunga mashine kisasa za Cyclotron, PET/CT Scan, MRI, na ICU. Aidha alisema ya kwamba dawa zote za tiba saratani zinapatikana kwa asilimia 98 na kushukuru Serikali kupeleka fedha MSD ili kununua dawa hizo.
Aidha , alizungumzia maandalizi ya kufungua kitengo cha upasuaji (surgical oncology) yanaendelea vizuri na yenye lengo la kuhakikisha huduma nyingi Kwa wagonjwa wa Saratani zinapatikani “chini ya paa moja” la hospitali hiyo