Mbunge wa Sengerema Tabasamu Hamis.
Mbunge wa Nyasa mkoani Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya
……………………………….
Na Selemani MSUYA
WABUNGE wa Bunge la Tanzania wamesema Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ukikamilika utakuwa fursa ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania.
Wabunge hao wamesema hayo baada ya kushuhudia zoezi la ujazaji maji wa bwawa hilo la kuzalisha umeme wa megawati 2,115 litakapokamilika.
Zoezi hilo la ujazaji maji JNHPP limefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Disemba 22,2022 ambapo viongozi na wananchi zaidi 2,000 walishuhudia.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande amesema ujenzi wa bwawa hilo la kisasa umefikia asilimia 78 na matarajio yao ni ifikapo 2025 Watanzania watakuwa wanapata umeme wa uhakika.
Mbunge wa Nyasa mkoani Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya amesema Mradi wa JNHPP unatarajiwa kutosheleza nchi na kuuza nje ya nchi, hali ambayo itakuza uchumi wa nchi na wananchi.
Amesema imani yake ni kwamba ongezeko la megawati 2,115 zitaweza kuchochea uwekezaji nchini kote kwa kuwa gharama itakuwa ndogo.
“Tunamshukuru Mungu kwa Mheshimiwa Rais Samia kuendeleza mradi huu, hii ndio tafsiri sahihi ya Tanzania na wengine katika kutambua michango ya watu wake, ni wazi kuwa vizazi vijavyo vitakuwa na taarifa rasmi ya mradi huo,”amesema.
Mhandisi Manyanya amesema ni wazi kuwa siku chache zijazo umeme hautakuwa kikwazo cha maendeleo.
Mbunge huyo amewataka Watanzania kutawanyika na kuwekeza katika maeneo mengine ili faida ya umeme huo iweze kupata.
“Mheshimiwa Rais Samia ameonesha dhamira yake ya kumaliza mradi huu na mimi nimekuwa nikisisitiza umalizike jambo ambalo kimenipa faraja,”amesema.
Naye Mbunge wa Sengerema Tabasamu Hamis amesema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa mradi huo kukamilika kwa asilimia 78 na kuwataka Watanzania waache kusikiliza porojo kwani kazi inaendelea.
Tabasamu amesema matarajio yake ni kuona gharama za umeme kushuka hali ambayo itaondoa malalamiko kuhusu gharama za nishati hiyo.
“Watanzania wasisikilize porojo, kwani kazi hapa JNHPP inaendelea, matarajio yetu ni gharama za nishati ya umeme kupungua mradi ukikamilika,”amesema.