Mwenyekiti wa Kituo cha Kutetea Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Mchange akizunguma katika mkutano na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam kuhusu utetezi wa rasilimali za nchi na mazingira klia ni Mjumbe wa MECIRA Irene Kilenga.
……………………………………
Na Selemani Msuya
MWENYEKITI wa Kituo cha Kutetea Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Mchange amewaomba Watanzania, asasi, mashirika na wadau mbalimbali kushiriki kutunza rasilimali misitu na kuhifadhi mazingira.
Mchange amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya taasisi hiyo kufanya kongamano la wadau wa habari mkoani Iringa.
Amesema kwa hatua iliyofikia kwenye uharibifu wa mazingira MECIRA hawatasubiri maelekezo ya waziri wa sekta husika ndio wachukue hatua.
Mwenyekiti huyo amesema kwa sasa inabidi kila mtanzania kushiriki kwa moyo mmoja kulinda mazingira ili nchi iwe salama.
“Sisi MECIRA katika hili tunaenda ulalo, ulalo kuhakisha mazingira yanakuwa salama, tunajua wapo watu wanakwazika na wengine kuleta propaganda katika jambo hili, hivyo watuchukie haturudi nyuma tutaendelea kupaza sauti.
Tumepata taaarifa huko Mto Ruvuma, Malagarasi na Kilombero hali sio shwari lakini sababu kubwa ni baadhi ya watu kushindwa kutimiza majukumu yao, lazima watu wabadilike,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema katika mapambano hayo wanatarajia kuanzisha tuzo kwa waandishi na vyombo vya habari ambavyo vinaandika habari za mazingira na uhifadhi.
Mchange amesema wao watasukuma ajenda kuhusu utunzaji wa mazingira, hivyo hawatarudi nyuma katika kusaidia nchi kupiga hatua za mazingira.