Asasi zisizo za kiserikali, wanasheria na wabia wa maendeleo wameaswa kuhakikisha kwamba katika shughuli zao za kila siku mtoto anazingatiwa katika shughuli zote zinazolenga kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko tabia nchi hasa kutatua changamoto za kimazingira.
Hayo yameelezwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Afisa miradi kutoka jukwaa la mabadiliko tabia nchi Forum CC Msololo Onditi wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya mradi inayolenga kuelezea athari za mabadiliko ya tabia kwa mtoto na haki zake.
Msololo Onditi amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi zinachangia kutokupatikana kwa usahihi kwa huduma za msingi kama huduma za Afya,Elimu,Miundombinu na Chakula.
” Tunapoongelea huduma hizi ni za msingi kwa mtoto, ni wakati sasa kwa wadau kuja pamoja na kuungana kuhakikisha kwamba mipango inayofanywa kwa kuangalia kutatua changamoto za kimazingira pamoja na kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi suala la mtoto liwe la msingi” alisema Msololo Onditi.
Kwa upande wake Justin Mponda kutoka taasisi ya Vijana amesema sheria ya mtoto ipo wazi lakini mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakiathiri moja kwa moja maendeleo ya watoto na vijana ambao ndio mustakabali wa taifa la sasa na la baadae na bila kujali kwamba kuna sheria.
Nae Witness Mosole ambaye ni wakili wa kujitegemea akizungumza katika uwasilishaji wa taarifa hiyo amesema kuna mapungufu ambayo yamejitokeza kwenye sheria zilizopo hususan kwenye namna ambayo mtoto anaweza akapata haki zake na kulindwa hasa kwenye changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo yapo na yanaendelea.
Mbali na hayo wakili Mosole amesema tafiti mbalimbali ikiwemo tafiti ya Shirika la Watoto Unicef ya 2017 inaonyesha watoto milioni mia sita hukumbwa na magonjwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, huku akibainisha kuwa sheria ya mtoto imeweka haki za mtoto na moja ya haki zake ni kupata elimu, kulindwa, maji safi na salama sheria ambazo zimekuwa kama hazitekelezwi.
Serikali ya Tanzania imeridhia itifaki mbalimbali za kimataifa ambazo zinalinda haki za binadamu na haki za mtoto.