………………….
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, leo tarehe 12 Desemba 2022, Jijini Arusha, amezindua Mkutano kuhusu Program ya kuwajengea uwezo wataalam chipukizi wa Afrika katika masuala ya Urithi wa Dunia na Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mkataba wa UNESCO wa 1972 ambao Tanzania imeridhia
Waziri Balozi Dkt. Chana, amesema kufanyika kwa Mkutano huo nchini ni matokeo chanya ya uongozi bora wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuzidi kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kuwa ni kisiwa cha amani, usalama na siasa safi.
Aidha, Mhe. Balozi Dkt. Chana ameongeza kuwa mkutano huo umelenga Kuwajengea uelewa wa pamoja wadau na watoa maamuzi juu ya kutekeleza, kubadilishana uzoefu na elimu ya Urithi wa Dunia, kuweka mkakati wa fursa kwa wote kuhusu Elimu na Ajira kwenye masuala ya Urithi pamoja na kuimarisha mtandao wa vyuo vikuu juu ya Urithi wa Afrika.
Waziri Balozi Dkt. Chana amesema kuwa, Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa Urithi wa Dunia hivyo amewashauri wajumbe wa Mkutano huo kuitumia fursa ya uwepo wao nchini kutembelea maeneo hayo na vivutio vingine.
Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana, ameushukuru uongozi wa Shirika hilo na wadau wa Urithi wa Dunia, kwa kuamua kufanyia Mkutano huo Tanzania kwani inasaidia kuongeza hamasa katika masuala ya Uhifadhi na kutoa wito kwa wadau wengine wa Kimataifa, kuja na kufanyia mikutano yao hapa nchini.