Mkurugenzi mtendaji wa TASESO ,Deus Lugaila akizungumza katika ufunguzi wa mkutano kwa wakuu wa shule,mameneja na wamiliki wa shule binafsi kanda ya kaskazini Magharibi .
…………….
Julieth Laizer,Arusha .
Arusha.Taasisi ya elimu (TASESO) wameiomba serikali kuwepo kwa ushirikiano wa kutosha kati ya shule binafsi na shule za umma ili mazuri yote yaliyopo shule binafsi yaende shule za umma na yaliyopo shule za umma yaende shule binafsi kwa maslahi mapana ya elimu ya nchi yetu.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi mtendaji wa TASESO,Deus Lugaila wakati akizungumza katika ufunguzi wa mkutano kwa wakuu wa shule,mameneja na wamiliki wa shule binafsi kanda ya kaskazini Magharibi.
Lugaila amesema kuwa,wameomba walimu wa shule za binafsi hasa wa shule za msingi wahusishwe moja kwa moja kwenye maswala yote ya kielimu na taaluma ya ualimu kwa ujumla kama semina za kiserikali nk.
Aidha wameomba kuwepo na uwezekano wa kuwaunganisha wamiliki wa shule binafsi nchini , wadau wa elimu na Serikali kuzungumza kwa kina juu ya masuala yote yahusuyo shule za binafsi nchini badala ya kutumia nyombo vya habari kutoa maelekezo yasiyo na majadiliano ya pande zote mbili.
“Tunaomba serikali ione namna ya kuwapunguzia au kuwafutia baadhi ya kodi zinazoumiza waajiri wa shule za binafsi katika uendeshaji wa shule zao kwa kuwa wao wanaendesha shule zao bila Suzuki kutoka serikalini ,hivyo kuathiri hata maslahi ya walimu ,hivyo tunaomba serikali iangalie utaratibu wa kuwasamehe wamiliki wa shule binafsi nchini malimbilizo ya kodi zote za nyuma za miaka 2015 hadi 2020.”amesema Lugaila.
Aidha amempongeza Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kulijenga Taifa letu na ushirikiano mkubwa wa karibu wanaopata katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku kama taasisi.
Amesema kuwa , tangu serikali iithibitishe taasisi hiyo wamefanikiwa kuratibu shughuli mbalimbali za kielimu ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kitaaluma kwa shule mbalimbali nchini ,uratibu wa shughuli za kitaaluma kama semina,uandaaji wa semina za kitaaluma kwa walimu, uandaaji wa kazi za likizo za nyumbani kwa wanafunzi pamoja na uandaaji wa mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi mashuleni ,uandaaji wa midahalo kwa wanafunzi mashuleni.
Aidha amesema kuwa,wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutoshirikishwa walimu wa shule za binafsi katika masuala muhimu ya kielimu yahusuyo elimu na walimu kwa ujumla kama semina za kiserikali, posho za mitihani ya serikali, pamoja na kurahisisha mitihani ya Taifa hasa shule za msingi.
Aidha amesema kuwa, changamoto nyingine ni pamoja na utitiri wa kodi za uendeshaji wa shule za binafsi nchini pamoja na shule binafsi kuchukuliwa kama washindani wa shule za serikali wakati ni wadau wa elimu wanaoshirikiana na kusaidiana na serikali katika kutoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania.
Kwa upande wake,Mkurugenzi mafunzo ya ualimu wizara ya elimu sayansi na Teknolojia, Huruma Mageni amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kutoa maoni ya uboreshaji wa mitaala ya elimu ngazi zote ambayo yanalenga kumwezesha mwanafunzi kuweza kujiajiri na kuajirika.
Mwisho.