Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo wa pili kushotoakipunga mkono kwa furaha na baadhi ya viongozi wa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO)ya Izazi Halmashauri ya wilaya Iringa wakati wa ziara yake ya kutembelea vyombo vya kutoa huduma na miradi ya maji inayotekelezwa katika mkoa wa Iringa.
Matenki mawili yanayotumika kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa kata ya Izazi wilayani Iringa ambayo yamesaidia sana kumaliza kero ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa kata hiyo.
Mwenyekiti wa Chombo cha kutoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO) ya Izazi Halmashauri ya wilaya ya Iringa Alamu Chanzi,akijaza maji kwenye madumu ya wananchi waliofika kupata huduma ya maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji katika kijiji hicho.
…………………
Na Muhidin Amri,
Iringa
MKURUGENZI Mkuu wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo amesema,kuanzia sasa Ruwasa itatoa Pikipiki na magari kwa vyombo vya kutoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO)vitakavyofanya vizuri kwenye makusanyo ya fedha za miradi ya maji.
Mhandisi Kivegalo amesema hayo jana,alipotembelea ofisi ya chombo cha kutoa huduma ya maji ngazi ya jamii katika kijiji cha Izazi kata ya Izazi Halmashauari ya wilaya Iringa mkoani Iringa akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Iringa.
Aidha alisema, Ruwasa itatoa vifaa vyote muhimu vya ofisi na kulipa mishahara ya miezi sita ya awali kwa wafanyakazi ili kuboresha utendaji kwa wafanyakazi wa vyombo hivyo ambavyo vina mchango mkubwa katika jamii hapa nchini.
Kivegalo,amewapongeza viongozi wa CBWSO hiyo kwa kufanya vizuri katika kuendesha mradi wa maji ambao umemaliza kero kwa wananchi wa kijiji cha Izazi kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji safi na salama.
“kihistoria Ruwasa tumekuwa wazuri katika kujenga miradi ya maji,lakini changamoto kubwa ipo kwenye uendeshaji wa miradi inayojengwa ,lakini Izazi mmefanikiwa sana katika uendeshaji wa mradi wa maji”alisema.
Hata hivyo,amewataka viongozi wa CBSWO kujipanga vizuri kwa kuongeza makusanyo ya fedha kutoka Sh.milioni 4 hadi kufikia milioni 8 kwa mwezi ili waweze kupanua mtandao na kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
Alisema,kama wakijipanga vizuri watakuwa na uwezo wa kuendesha mradi huo bila kutegemea ruzuku na msaada wa fedha kutoka serikalini kwa kuwa makusanyo yatakayopatikana yatatumika kuboresha huduma,kukarabati miundombinu na kupunguza upoteza wa maji.
“nikija tena baada ya miezi sita nisikie makusanyo ya fedha yamefikia milioni 6 hadi 8 badala ya kubaki na kiwango cha Sh.milioni na uwezo huo mnao, kwa hiyo Mwenyekiti na timu yako nawaomba sana ongezeni jitihada na naamini mtafanikiwa”alisema Kivegalo.
Pia,amewataka viongozi wa CBSWO hiyo kutumia makusanyo ya fedha zinazotokana na mauzo ya maji kupanua mtandao na kuboresha huduma ya maji ili wananchi waweze kupata huduma umbali usiozidi mita 400.
Mwenyekiti wa CBSWO hiyo Alamu Chanzi alisema,zaidi ya watu 6,670 wamenufaika na mradi huo na kati ya hao watu 4,700 wanapata huduma ya maji safi na salama huku baadhi yao tayari wameshavuta maji kwenye nyumba zao.
Chanzi alieleza kuwa,kabla ya kuanzishwa kwa chombo hicho wananchi wa kijiji cha Izazi,Mnadani na Makuka walisumbuliwa na magonjwa ya mara kwa mara kama matumbo na kuhara kutokana na kutumia maji ya Bwawa la Mtera ambayo sio safi na salama.
Alisema,baada ya mradi huo sasa afya za wananchi wa vijiji hivyo zimeimarika na wanapata muda mwingi wa kufanya shughuli zao za maendeleo na kupunguza gharama za matibabu.
Kwa upande wake Mhasibu wa CBWSO ya Izazi Christina Sanga alisema,kabla ya kuanzishwa chombo hicho huduma ya maji ilitolewa bila utaratibu maalum na hivyo kusababisha huduma ya maji kutokuwa ya uhakika na wananchi kushindwa kupata huduma hasa pale miundombinu inapo haribika na kushindwa kufanyiwa matengenezo kwa wakati.
Alisema,baada ya kuanzishwa CBWSO sasa mapato ya fedha yanaonekana na mradi unaendeshwa vizuri kwa kuwa hata miundombinu inapoharibika inafanyiwa matengenezo haraka ikilinganishwa na hapo awali.
MWISHO.