……………………..
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefanya ufatiliaji wa utekelezaji wa Miradi ya Kimaendeleo yenye thamani ya bilioni 2.3.
Akizungumza na waandishi wa habari leo November 29, 2022 kuhusu taarifa ya utendaji kuanzia Mwezi Julia hadi September 2022, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Eugenius Hazinamwisho, amesema kuwa wamefatilia utekelezaji wa miradi 12 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 katika sekta za Ujenzi, Elimu, Masoko, Maendeleo ya Jamii pamoja na Afya.
Bw. Hazinamwisho amesema kuwa miradi waliofatilia inajumuisha miradi ya mipango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19.
“Baadhi ya miradi ilionekana kuwa na mapungufu ikiwemo kuchelewa kukamilika kwa mujibu wa mkataba jambo linalosababisha kuongezeka kwa gharama, vifaa visivyokidhi ubora pamoja na manunuzi kwa gharama zaidi ya bei ya soko” amesema Bw. Hazinamwisho.
Amebainisha kuwa baadhi ya miradi ilionekana kuwa na dosari ni Ujenzi wa wodi ya mama na mtoto, Zahanati ya Mbande Kata ya Chamazi ambapo kuna ubovu wa milango na vyoo.
Ujenzi wa madarasa 13 na matundu ya vyoo 16 katika Shule ya Msingi Goroka “A” ambapo Ujenzi wake umeonekana kuwa duni pamoja na ucheleweshaji wa malipo ya fundi.
Ujenzi wa soko la Buza Stand ambapo kulikuwa na ukikwaji wa mwongozo wa utekelezaji wa miradi kwa njia Force Account (Fundi aliyepewa kazi ya Ujenzi ndiye Supplier wa vifaa vya Ujenzi).
Bw. Hazinamwisho amebainisha kuwa katika sekta ya manunuzi ya umma wamebaini mwongozo wa matumizi ya Force Account haufuatwi pamoja na hakuna ushindani wazabuni wa vifaa na mafundi.
Ameeleza kuwa katika uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki, Halmshauri ya Manispaa ya Kigamboni imebainika kuwepo kwa mashine takribani 27 ambazo hazitumiko kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa ubovu wa mashine.
“Pia Kuna mikataba ya wazabuni imeshaisha muda lakini wazabuni bado wanaendelea na kazi huku wakiwa hawajasaini mikataba mipya kinyume na sheria na taratibu za ajira na sheria za ukusanyaji mapato” amesema Bw. Hazinamwisho.
Katika hatua nyengine ameeleza kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu vitendo vya rushwa jambo ambalo litasaidia kuimarisha vitendo juhudi za Kuzuia rushwa kwa Kufatilia utekelezaji wa miradi ya Kimaendeleo.
“Tunawashukuru wananchi wa Mkoa wa Temeke kwa kutuunga mkono katika vita ya Kuzuia vitendo vya rushwa” amesema Bw. Hazinamwisho.