………………………
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement KIVEGALO ameonesha kutoridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji Mtiririko kwa Vijiji viwili vya Malangali na Hanjawanu (Igando-Kijombe) Wilayani Wanging’ombe Mkoa wa Njombe.
Akiwa katika ziara yake na wataalamu kutoka RUWASA Makao Makuu amesema mradi huu ni wa muda mrefu na ulirithiwa kutoka halmashauri kabla ya kuanzishwa kwa RUWASA lakini ubora na utekelezaji wa mradi sio wa kiwango kizuri.
Sijaridhishwa na utekelezaji wa huu Mradi, STC ni Kampuni kubwa ya daraja A lakini kazi yao siyo nzuri katika mradi huu. Nakuagiza Mkurugenzi wa Ufundi – RUWASA urudi kwenye mradi huu ukae na mkandarasi mpitie kipengele kwa kipengele cha mkata na mapungufu yote yarekebishwe kwa gharama za Mkandarasi”. Alisema Kivegalo.
Mradi wa maji mtiririko wa Igando Kijombe ni mradi uliosanifiwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa vijiji 10 wilayani Wanging’ombe vya Malangali, Wangamiko, Mpanga, Luduga, Hanjawanu, Igando, Iyayi, Lyadebwe, Mayale na Kijombe vyenye wakazi wapatao 14,377.
Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya M/S STC JV YELL LTD kwa gharama ya shilingi 12,437,407,360.00 fedha za ndani kupitia Mfuko wa Maji (NWF).
Kazi zilizopangwa kutekelezwa hadi sasa ni Ujenzi wa mtego wa kuchotea maji (intake) katika kijito cha Ng’engemala – kijiji cha Malangali, Ujenzi wa chujio katika kijiji cha Malangali, Ujenzi wa bomba kuu umbali wa kilomita 28.940, Ujenzi wa mabomba ya usambazaji wa maji kilomita 18.238, Ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji juu ya ardhi lenye ujazo wa lita 150,000 katika kijiji cha Malangali, Ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika kijiji cha Malangali (eneo la chujio).
Kazi nyingine ni Ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 100,000 juu mnara wa mita 9 katika kijiji cha Hanjawanu, Ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 22, Ujenzi wa mabakuli mawili ya kunywea maji mifugo (cattle trough) na Ujenzi wa miundombinu mitatu ya kuchotea maji ya mvua.
Mradi huo sasa upo asilimia 86 ya utekelezaji na unapaswa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2022.