Mwenyekiti wa Kijiji Cha Nambinda Said Abdala Kowe akizungumza na waandishi wa habari za Utunzaji wa misitu ya asili ya vijiji na maofisa wa shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) walipometembelea kijiji hicho wilayani Liwale mkoani Lindi.
…………………………….
Serikali imeombwa kukiunga Mkono Kijiji Cha Nambinda kilichopo katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi katika kufanikisha utekeleza wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo Ujenzi wa kituo Cha Afya.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kijiji Cha Nambinda Said Abdala Kowe wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wametembelea kijiji hicho wakiongozana na maofisa wa shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) ambapo amesema kuwa kutokana na changamoto waliyokuwa wanaipata ya kituo cha Afya wameamua kujenga zahanati ili kurahisisha huduma hiyo.
Kowe amesema kuwa kupitia rasilimali misitu zilizopo kwenye Kijiji hicho wametumia Mill 33 kwa ajili ya kujenga zahanati jambo ambalo litaondoa changamoto iliyokuwa inawakabili ya kwenda umbali mrefu hususani wakina mama wamekuwa wakiteseka.
“Kutokana na kutokuwepo kwa zahanati katika kijiji chetu tulikuwa tunapata athari Kubwa sana maana tulikuwa tunaenda umbali wa kilomita nane hali ambayo tumepoteza watu wengi sana Kwa wagonjwa kufariki baada ya kucheleweshwa kupata matibabu”amesema Kowe
Amesema wamefarijika Kwa ujio wa Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) jambo lililowafanya kupata fedha za kuendeleza miradi katika kijiji chao hivyo wameiomba serikali kuwaunga mkono waweze kupata kituo Cha Afya kwani sera ya nchi inasema katika kila kata kuwe na kituo hicho.
“Naishauri serikali itusaidie katika ufanikishaji wa Mradi huu kwani tulikuwa na mwanakikundi mwenzetu wa Mkaa Endelevu Mmoja amepoteza Maisha akiwa mjamzito na wakati wanampeleka kituo cha afya hakufika Kwenye Kilomita nane akafariki Njiani”ameendelea kusema Mwenyekiti Kowe
Mwenyekiti Kowe amesema licha ya kwamba mradi huo walitakiwa kukamilisha Mwezi wa kumi pamoja na kusuasua kwa Fedha wanatarajia kukamilisha Mwezi wa kwanza Mwaka ujao.
Kuhusu utofauti ulipo baina ya Kijiji hicho na vingine Kowe amesema kuwa wamekuwa wa mfano katika kuhakikisha wanafanikisha Maendeleo ikiwemo mchango walioutoa kujenga vyoo vya Hostel ya sekondari yao ya kata.
Kowe amepongeza mashirika ya kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) kwa kuwaletea Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) kwani mradi huo umesaidia sana kuwapa uelewa mpana juu ya umuhimu wa rasilimali za misitu ambazo zimeanza kuwaletea maendeleo katika kijiji chao na mwananchi mmoja mmoja.
Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) ambao unafikia ukingoni mwishoni mwa mwezi huu ulikuwa unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC).
Jengo la Zahanati ya kijiji cha Nambinda ambalo ujenzi wake umenzishwa kwa fedha za rasirimali za misitu ya kijiji hicho linavyoonekana baada ya ujenzi huo kuanza.
Saidi Abdalla Barabara Katibu wa Kamati ya Maliasili kijiji cha Nambinda akisoma taarifa ya matumizi na mapato ya kijiji hicho.
Bettie Luwuge Afisa Mawasiliano wa shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania TFCG akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nambinda wakati alipowatembelea kukagua miradi ya maendeleo inayotokana na rasirimali za misitu kijijini hapo.
Celina Mlelwa Afisa Habari wa wilaya ya Liwale akizungumza katika kikao hicho.
Lilian Kato Afisa Misitu wilaya ya Liwale akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya mambo kwa waandishi wa katika kikao kilichofanyika kijijini hapo.
Lilian Kato Afisa Misitu wilaya ya Liwale akizungumza na waandishi wa habari kando ya bwawa la Okororo linalohifadhiwa katika msitu wa kijiji cha Nambinda.
Kwa mbali ni baadhi ya viboko wanaopatikana katika bwawa hilo ambalo limekuwa k.imbilio kwa wanyama kujipatia maji ya kunywa hasa kwa kipindi hiki cha kiangazi.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Nambinda akilielezea Bwawa la Okororo na faida zake ambapo kutokana na mila na desturi za kabila la Kingindo pamekuwa pakifanyika matambiko ya mambo mbalimbali katika bwawa hilo ambalo amesema lina faida kubwa kwao.
Mkurugenzi wa Fullshangwe Bw. John Bukuku akiwa na mmoja wa wanahabari wa TBC Bw. Bahule Mnyonge kando ya Bwawa hilo ambalo linafaa sana kwa utalii wa ndani.