…………………
Na Farida Mangube,Morogoro.
Ongezeko na kukithili kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini hasa kwa wanawake na watoto kumechangia migogoro ya kifamilia, talaka na kukosekana kwa malezi ya dhati kutoka kwa wazazi na walezi na kufanya watoto kuishi mazingira hatarishi na mwingine kwenye vituo vya kulelea watoto.
Carolyn Kezilahabi anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 14 mzaliwa wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, kwasasa anaishi kituo cha Raya Orphanage Centre kilichopo Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, baada ya kuchoshwa na manyanyaso na vipigo vya kila uchwao kutoka kwa Shangazi yake.
Anasema miaka mitano iliyopita shangazi yake alifika kijijini kwao na kumchukua kuja kuishi nae Dakawa Wilayani Mvomero baada ya Bibi yake kufariki, shangazi huyo alimuahidi kumuendeleza kimasomo, lakini walipofika Dakawa imekuwa tofauti.
Anasema baada ya kufika Dakawa shangazi yake alianza kumnyanyasa na kumtesa kwa kumpatia kikombe kimoja cha chai na chapati moja kama chakula cha siku nzima.
“Shangazi yangu alikuwa nafanya biashara ya kupika chai siku moja nilikuwa namimina chai kwa bahati mbaya nikadondosha chupa ya chai na ikavunjika nikamwambia shangazi chupa imevunjika lakini hakunielewa akaanza kunipiga na flampeni kichwani, na baadae kuchukua panga, aliponyanyua panga kutaka kunipiga kichwani nikaweka mkono na akanikata kwenye kidole.”alisema Carolyn
Aidha anasema baada ya kipigo hicho alikimbia na kwenda kumueleza Mwalimu wake shule ya msingi dakawa alipokuwa anasoma ambaye alimpeleka kwa Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa na kuweza kupata hifadhi kwa muda na ndipo safari yake ya kuanza kuishi kwenye kituo cha kulelea watoto cha Raya Orphanage Centre.
Mtoto huyo kwa sasa kilio chake kikubwa anatamani kukutana na kuwaona wazazi wake ambao hajawaona wala kuwasikia hata kwa simu kwa zaidi ya miaka mitano na kwamba sababu aliondoka Ukelewe akiwa katika umri mdogo hivyo anashindwa kukumbuka amezaliwa kijiji gani.
Kilio cha Carolyn ambaye amehitimu darasa la saba na anasubiri matokeo kwa sasa,kimekuja baada viongozi wa Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Kamishna wa forodha na ushuru wa bidhaa wa TRA makao makuu Said Kiondo kutembelea kituo cha Raya wakati wa maadhimisho ya wiki ya mlipa kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamishna huyo Kiondo alisema TRA imeona ni vyema kurudisha faida kwa jamii ambayo imekuwa mstari wa mbele kwenye ulipaji wa kodi.
Aidha aliwataka watanzania kuendelea na utamaduni wa kudai lisiti halali za bidhaa wanazonunua ili kustawisha uchumi wa nchi kwani wanabaadhi ya wafanyabishara wamekuwa tabia ya kutoa risiti tofauti na kiasi kilicholipwa na mteja.
Pia amewataka wafanyabiashara kuwasilisha litani zao ndani ya muda uliopangwa kisheria kwani kwa kuchelewesha kupeleka litani ndani kunapelekea usumbufu pamoja na kupigwa faini jambo ambalo linamfanya mfanyabiashara kuongeza gharama kwenye biashara yake.
Kiondo aliwataka Wananchi kulipa kodi kwa wakati kwani Tra kodi zake zimepangwa kwa wakati na kuna kodi za siku, mwezi, robo ya mwaka na mwaka moja hivyo akawasisitiza wananchi kulipa kodi hizo kwa wakati kunaisaidia TRA kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto yatima cha Raya Orphanage Raya Subaha aliishukuru TRA Mkoa wa Morogoro kwa kuwatembelea na kuwafariji watoto waishio katika kituo hicho na kwamba kwa sasa analea watoto 70.
Alisema hicho kituo kimekuwa kikiwajengea watoto uwezo wa kujitambu kwa kuwafundisha elimu ya dini pamoja na ile ya dunia na watoto wanakabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufika shuleni huku kipindi cha mvua kutokana na mito kujaa maji watoto ushindwa kuhudhuria masomo..
TRA Mkoa wa Morogoro katika kuadhimisha wiki ya mlipa kodi wamefanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa walipa kodi pamoja na kurejesha faida ya sehemu ya mapato yake katika jamii, kwa kutembelea vituo vya kulea watoto na kutoa mahitaji mbalimbali ambapo wametembelea kituo cha Mgolole pamoja na Raya vyote vya kulelea watoto yatima na waliotelekezwa na wazazi wao ambapo waliwapatia zawadi mbalimbali.
Mwisho.