Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja wakati akizungumza katika warsha iliyowakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujadili urejeshaji wa uoto wa asili.
Kamisha wa Uhifadhi wa wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Dos santos Silayo katika warsha iliyowakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujadili urejeshaji wa uoto wa asili.
…………………
NA MUSSA KHALID
Serikali imeweka mpango mkakati wa kuhakikisha mpaka kufika mwaka 2030 uoto wa asili uwe umerejeshwa kwa Jumla ya Hekta Mill 5.2.
Kauli hiyo imelezwa leo jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja wakati akizungumza katika warsha iliyowakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujadili urejeshaji wa uoto wa asili.
Naibu Waziri Masanja amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 ambazo zimetakiwa kuingia kwenye mkataba wa urejeshaji wa uoto wa asili ambapo nchi 32 tayari zimesaini mkataba huo.
‘Malengo ya dunia ni kuhakikisha kwamba Jumla ya Hekta Mill 350 zinarudi kwenye uoto wa asili lakini kwa Afrika tuna malengo ya Jumla ya Hekta Mill 100 ambazo zinatakiwa zirejeshwe kwenye uoto wa asili na kwanza Tanzania tumeweka malengo ya kuwa tunarejesha jumla ya hekta Mill 5.2 na mpango huu tuliuweka tangu mwaka 2018’amesema Naibu Waziri Masanja
Amesema kupitia mpango huo serikali imekuwa ikitoa elimu kwa watu mbalimbali ili waweze kuingia kwenye mpango huo ambao pia awali walikwisha tambua kuna baadhi ya maeneo ambayo tayari yamevamiwa na wananchi na yalistahili kuhifadhiwa vizuri.
Aidha amesema kuwa kutokana na kuwa kwa sasa hali siyo nzuri wameanza kuchukua hatua za haraka za kuielimisha jamii kujua namna bora ya utunzaji wa misitu na uvunaji usiokuwa holela.
Kwa upande wake Kamisha wa Uhifadhi wa wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Dos santos Silayo amesema kuwa lengo la serikali ni kurejesha uoto ikiwa ni pamoja na kuzuia uharibifu wa maeneo ya misitu nchini.
‘Mkakati huu unalenga sio kuboresha tu mazingira yaliyoharibika lakini ni kuhakikisha kwamba jamii zinazoishi maeneo mbalimbali wanategemea mazingira ya kuishi zinaweza kujiinua kiuchumi hivyo kunyanya uwezo wa wananchi ni miongoni mwa shughuli ambayo serikali imejiwekea malengo ili kuboresha maisha ya wananchi’amesema Prof Dosantos
Winifrida Jackson ni Balozi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira amesema ni vyema kila mtu akaongeza jitihada katika utunzanji wa wa mazingira huku Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania Dkt Revocatus Mushumbus amesema miti ming I imetoweka kutokana na shughuli za binadamu.
Katika warsha hiyo wamehudhuria wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kuangalia na kujadili namna ya urejeshaji wa uoto wa asili katika nchi zao.